Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini ambao bado hawajaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 wawe wameshaanzisha kabla ya mwaka 2024.
Majaliwa pia amewataka Viongozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi waimarishe huduma za uwezeshaji ili waweze kuyafikia malengo waliojiwekea na kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwezeshaji na kupunguza umaskini nchini.
Ameyatoa maagizo hayo wakati akifunga Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na kusema “Suala la kuanzisha vituo vya uwezeshaji ni maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 katika Ibara ya 26 (k) na hili ni jukumu letu viongozi kuhakiksha ilani inatekelezwa.”
Aidha, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa mikoa na halmashauri zote nchini wahakikishe wanaimarisha Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ambazo zitawaongezea kipato.
“Katika hili ninawapongeza Mkoa wa Dodoma kwa kuwezesha Jukwaa la Mkoa kuanzisha SACCOs 76 za wanawake zenye wanachama 322 pamoja na Halmashauri ya Ushetu ambayo imeanzisha Jukwaa linaloendesha Mradi wa Kampuni ya Usafi wa Mazingira na usindikaji wa mboga za majani maarufu kwa jina la Nsansa,” alisisitiza Waziri Mkuu.