Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Eng. Tumaini Magesa na Mkurugenzi wa Halmsahuri ya wilaya hiyo, Tamim Kambona kufika kata ya Engusero Jumamosi wiki hii wakafanye mkutano wa hadhara na kujibu kero za wananchi wa kata hiyo.
Mkuu wa Wilaya hiyo na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo wametakiwa pia wafuatane na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Lairumbe Mollel wakatoe ufafanuzi kwa wananchi bila kukosa kuhusu gari la wagonjwa lililokuwepo na sasa halipo.
”Nataka wawaambie gari hilo liko wapi na linafanya nini” – amesisitiza
Majaliwa ametoa agizo hilo lei Februari 15, 2017 katika kijiji cha Engusero wilayani kiteto baada ya kusimamishwa na wananchi wakati akiwa njiani kuelekea mjini Kibaya yalipo makao makuu ya wilaya hiyo ili aanze ziara ya kikazi ya mkoa wa Manyara.
“Nitaawagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri waje hapa Jumamosi hii na kufanya mkutano ili wawaeleze wana mpango gani kuhusiana na ujenzi wa soko hilo,” amesema.
Awali , Mkazi wa kata hiyo, Ali Athumani alimuomba Waziri Mkuu awasiaidie ili wajengewe soko la kimataifa kwa sababu wao ni wazalishaji wakubwa wa mahindi lakini hawafaidiki nayo kwa sababu yote yanaenda kuuzwa katika soko la Kibaigwa.