Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewashukuru Watanzania wote kwa kuonesha mshikamano na uzalendo wa hali ya juu wakati wa kutangazwa na kipindi chote cha maombolezo ya msiba hadi mazishi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, April 07,2021 katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma akitokea Visiwani Zanzibar katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Abeid Aman Karume.

Majaliwa amewashukuru Watanzania wote kwa namna walivyoshiriki katika zoezi hilo, na kuwaomba waendeleze utulivu na mshikamano mkubwa waliounesha katika kipindi chote cha majonzi.

“Wakati wote tangu msiba ulipotangazwa Watanzania walikuwa watulivu hadi leo tunapomaliza siku 21 za maombolezo, tunawashukuru sana,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa miongozo yake aliyoitoa ambayo iliiwezesha kamati ya mazishi ya kitaifa kuratibu vizuri zoezi hilo na kufanikisha mazishi ya Hayati Dkt. Magufuli.

“Kauli yake iliwasaidia Watanzania kuendelea kuwa watulivu huku wakimuombea Hayati Dkt. Magufuli,” ameongeza Waziri Mkuu.

Baraza, Kagera Sugar majaribuni Mbeya
Ndumbaro kushughulikia makazi hifadhi ya Ngorongoro