Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa tahadhari kwa wadau wote wa madini kuwa atakayekamatwa anatorosha madini, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo utaifishaji wa madini atakayokuwa akiyatorosha.
Majaliwa ametoa tahadhari hiyo leo Machi 17, 2019 wakati akifungua soko la madini la Mkoa wa Geita. Ufunguzi wa soko hilo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilotoa tarehe 22.01.2019 la kuitaka mikoa yote ianzishe masoko ya madini.
Pia amewataka viongozi na watendaji wote wa Serikali wasimamie kwa weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo kuhusu sekta ya madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususan dhahabu kwenda nje ya nchi.
Ameitaka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Serikali ya Mkoa, Idara na Taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na maendeleo ya sekta ya madini waheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri soko hilo na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.
“Wizara ya Madini ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuandaa mpango kazi mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hili ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabishara wa madini”
Waziri Mkuu ameviagizaVyombo vya Ulinzi na Usalama vihakishe soko hilo linapata ulinzi wa kutosha muda wote ili watendaji, mali zitakazokuwemo, vitendea kazi na miundombinu yote iwe salama muda wote. “Mkuu wa mkoa na Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nawaagiza hakikisheni Suala hili mnaliandalia utaratibu haraka iwezekanavyo”.