Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim majaliwa amewataka Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) wakutane na wamiliki wa taasisi za kifedha ili kuwasaidia wananchi kupata mikopo yenye masharti nafuu itakayowawezesha kukuza uchumi wao.
Majaliwa amesema hayo leo Januari 24, 2017 wakati alipokutana na wajumbe wa baraza hilo katika Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
“Baraza likutane na wamiliki hao na kuzungumza namna sahihi ya kuwezesha kutoa mikopo ya masharti nafuu. Pia tuangalie taasisi hizo zinatuasadiaje sisi kama Serikali kuwawezesha Watanzania kupata mikopo ya masharti nafuu,” amesema.
Majaliwa amesema wananchi wanahitaji kuona ni namna gani Serikali imejipanga kuwawezesha wao kiuchumi, hivyo baraza litoe muelekeo wa namna ya wananchi watakavyoweza kufuga na kulima kitaalam ili waweze kupata tija kwani asilimia 80 ya wananchi wanajishughulisha na kilimo kama njia sahihi ya kuboresha uchumi. Pia ufugaji unaweza kusaidia jamii ya wafugaji kupata tija, hivyo baraza liwasaidie kwa kuwapa mbinu sahihi za kuboresha ufugaji wao.
Naye Mwenyekiti wa baraza hilo, Dk. John Jingu amesema baraza lilizinduliwa Januari 8, 2017 na walikubaliana kuanza kazi katika maeneo ya kipaumbele yatakayokuwa na tija kwa wananchi ambayo ni kilimo, sanaa, ufugaji na uvuvi.
Dkt. Jingu amesema kinachotakiwa kwa sasa ni kutafuta mbinu zitakazoweza kutatua changamoto kubwa zinazowakabili ambazo ni pamoja na ukosefu wa mitaji na masoko ya uhakika kwa mazao yao.