Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Watanzania wanatakiwa kuiamini Serikali ya Awamu ya Tano kwani imevipa muda vyombo vya dola kufanya uchunguzi dhidi ya matukio ya kihalifu yanayoendelea kutokea hapa nchini.
Majaliwa amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa pindi yanapotokea matukio ya kihalifu.
Ameyasema hayo mapema hii leo Bungeni Mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kupata kauli ya Serikali juu ya hofu iliyotawala nchini kuhusu vitendo vya watu kihalifu, kupotea na kutekwa.
“Tukitoa taarifa mapema tunaweza kuharibu upelelezi, tuviachie vyombo vyetu vya dola viendelee kufuatilia kuona nani anayesababisha vitendo hivyo na dosari iko wapi na nini chanzo chake,”amesema Majaliwa.
Majaliwa amewasihi Watanzania kuendeleza utamaduni mzuri wa watu kuheshimiana, kufuata kanuni na kuviachia vyombo vya dola kutekeleza majukumu yake.
Aidha, ameongeza kuwa vyombo vya dola vina weledi, vifaa na uwezo wa kutosha kufanya uchunguzi juu mambo yanayotokea nchini hivyo amesisitiza wananchi kuendelea kuiamini Serikali kwani matukio ya kihalifu likiwemo la mtu kutoweka au kufariki huwa hayana ukomo wa uchunguzi.
Hata hivyo katika hatua nyingine, Majaliwa amesema Serikali inafanya mapitio kwa vyama vyote vya Ushirika nchini kufuatia baadhi ya vyama hivyo kuwa na mwenendo mbaya hali inayochangia upotevu wa fedha nyingi na kukatisha tamaa wakulima.