Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa sukari iliyoagizwa na wafanyabiashara waliopewa vibali vya kuuza nchini itakuwa imeisha kipindi cha mwezi wa Ramadhani utakapoanza na kuwa bei itakuwa imepungua.
Ameyasema hayo mapema hii leo bungeni mjini Dodoma wakati wa maswali na majibu, amesema kuwa kuhusu kupungua kwa sukari nchini na mahitaji yake Serikali iko macho na itahakikisha inafanya jitihada za upatikanaji wa mahitaji yote ya msingi.
“Mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 lakini kwa sasa tunazalisha tani 320,000 hivyo mwaka huu Serikali imeagiza tani 80,000 na tayari tani 35,000 zimeshaingizwa nchini,”amesema Majaliwa.
Hata hivyo, Majaliwa amewasihi wafanyabiashara kushusha bei ya sukari waliyoipandisha kwani Serikali inashirikiana nao ili kuweza kuweka mazingira rafiki kwa wananchi.