Tanzania inaendelea kupata sifa kubwa za ukarimu, amani, upendo na utulivu duniani, sifa ambazo zinazidi kujidhihirisha kila kunapokucha huku nchi nyingi duniani zikiendelea kutamani kinachoendelea nchini wakiomba kitokee nchini kwao pia.

Miezi michache, joto la kampeni na mvutano mkubwa wa nguvu ya wagombea na vyama vilivyokuwa vinashiriki uchaguzi Mkuu zilipelekea baadhi ya watu kuamini kuwa huenda uchaguzi ungeisha huku sifa ya ‘Tanzania kuwa kisiwa cha amani na utulivu’ ikipata doa.

Lakini Busara za viongozi wa vyama vya siasa na serikali na maombi ya viongozi wa dini zote zilituvusha salama na joto hilo la uchaguzi limekwisha ndani ya muda mfupi na sasa ni ‘Kazi Tu’ na kushindana kwa hoja kujenga nchi.

Jana, kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowassa alikutana kwa mara ya kwanza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo. Wawili hao walikutana katika ibada maalum ya kumuingiza kazini Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo iliyofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Picha za tukio la kusalimiana kati ya wawili hao zinaongea lugha kubwa inayoakisi sifa nzuri ya Tanzania na upekee wake hususan katika bara la Afrika ambalo uhasimu wa kisiasa huvuka mipaka.

Viongozi hao walionekana wenye furaha, waliochangamkiana na kucheka kwa pamoja kuashiria kuwa salamu yao ilitawaliwa na furaha kubwa.

Bila shaka, Lowassa alimpongeza Majaliwa kwa kushika nafasi hiyo ambayo yeye aliwahi kuishika na kujiuzulu miaka michache baadaye kutokana na kukumbwa na kashfa ya Richmond. Bila shaka alimtakia heri katika utendaji wake wa kazi.

Taswira hii inayoonekana kutoka kwa viongozi wetu ambao ni mahasimu wa kisiasa ni muhimu sana kwa mustakabali wa taifa letu kuwa uhasama wa kisiasa ulenge katika kutofautiana kimtazamo na itikadi tu na sio zaidi ya hapo kwani pande zote zina lengo la kujenga Taifa na kuleta maendeleo zaidi.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli, Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa serikali walifika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kumjulia hali Waziri Mkuu mstaafu aliyekuwa kinara wa kunadi sera za Chadema na kukosoa serikali ya CCM katika uchaguzi Mkuu, Frederick Sumaye.

Wananchi tunapaswa kujifunza kupitia viongozi wetu, amani na utulivu mbele kwakuwa tunajenga nyumba moja, tusiruhusu mwanya wa kugombea fito.

 

Ruby amlilia Ali Kiba, adai amemfananisha na Mbwa
Majipu, Mbwa na Askari Bungeni vyamgusa Askofu Mkuu KKKT