Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza mifumo ya utoaji huduma Serikali kwa njia ya mitandao isitumike kukwamisha shughuli za Serikali au mipango ya utoaji huduma kwa wananchi.
Majaliwa amesema hayo mara baada ya kuzindua mifumo tisa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dodoma.
Amesema kuwa watakaobainika kuhujumu mifumo hiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu na amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haitawavumilia watumishi wasio waadilifu.
Amesema lengo la Serikali la kutumia mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.
“Hivyo basi, mtakubaliana nami kuwa, Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azma ya kuwapatia wananchi hususani wa vijijini huduma bora na kwa wakati,” amesema.
Aidha, Majaliwa ametoa wito kwa Watumishi wa Umma wote nchini, wananchi, Sekta Binafsi, Sekta ya Umma, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kisiasa na Wadau mbalimbali, kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa.
“Hii ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo Malengo ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika (AU) na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 ya Umoja wa Mataifa ambayo yamehimizwa na Kaulimbiu ya mwaka huu,”.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza Watendaji Wakuu wa Taasisi zinazosimamia mifumo hiyo pamoja na maafisa waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi kupitia mifumo hiyo, wahakikisha wanailinda na kuitumia vema ili iweze kuwa na tija na manufaa yaliyokusudiwa.