Katika kuhakikisha kuwa sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinafaana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefanya ukaguzi wa miundombinu na kusema kuwa maandalizi yake yako vizuri.
Ameyasema hayo mapema hii leo katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa ya maandalizi ambapo kunatarajiwa kuwepo kwa burudani mbalimbali.
“Tunatarajia wageni wengi kutoka nje ya mkoa huu wakiwemo viongozi wastaafu wa kitaifa, waheshimiwa mabalozi na wake wa waasisi wa Taifa hili, Mama Maria Nyerere na Mama Fatma Karume. Pia tutawatambulisha rasmi ndugu zetu waliochanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964,” amesema Majaliwa.
Aidha, Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wakazi kutoka wilaya zote za mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani wafike kwenye maonyesho hayo ambayo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania yanafanyika mkoani humo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba sehemu zilizobakia zitakamilika kabla ya kesho.