Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha uhusiano wa kimataifa ili kuchochea uwekezaji na kukuza uchumi wa Nchi.
“Rais ameniagiza niwaambie kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kuwapokea, kuwasikiliza na kushirikiana nanyi katika kuimarisha shughuli za uwekezaji na biashara nchini.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 16, 2021 wakati akifungua kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo amesema katika kipindi kifupi Rais Samia ameboresha mahusiano na Nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza uchumi.
Amesema Rais Samia ameongeza usimamizi wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha zenye mwelekeo wa kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ambapo katika kipindi cha Machi hadi Agosti 2021, Tanzania imeongoza kwa kuvutia kiwango kikubwa zaidi cha uwekezaji kutoka nje kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kiwango cha uwekezaji kutoka nje kilifikia USD bilioni 2.9.