Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Novemba 16, 2021 amezindua kiwanda cha SIKA kinachotengeneza na kusambaza bidhaa zitumikazo kwenye ujenzi wa majengo, miundombinu pamoja na kwenye viwanda vya utengenezaji (magari, mabasi, lori, reli, mitambo ya nishati ya jua na upepo, facade.
Akiwa kiwandani hapo Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na hivyo kuwezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Majaliwa pia ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara iendelee na uratibu wa kukutana na Wizara au Taasisi za Serikali na Binafsi nchini ili kuwahamasisha kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Waziri Mkuu pia amewataka wamiliki wa viwanda nchini wawe tayari kuwapokea na kuwapa ushirikiano Watu wenye ulemavu ili waweze kupata fursa ya kuchangia katika shughuli za ujenzi wa Taifa kama Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini inavyotutaka.
Aidha, ametoa wito kwa Wafanyakazi wa kiwanda hicho wamsaidie muwekezaji ili akuze zaidi biashara yake na anufaike na uwekezaji huo.
“Kila mmoja asaidie ulinzi wa mali za kampuni, msikubali kushawishika kuhujumu kiwanda hiki, kinamanufaa kwetu” amesema Majaliwa.