Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwaua majambazi watano na kukamata silaha moja bastola aina ya STAR iliyofutwa namba ikiwa na risasi tatu ndani, kasha(Magazine) na maganda mawili ya risasi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa, mnamo tarehe 27/02/2021 majira ya saa kumi na mbili asubuhi maeneo ya Kivule kwa Iranga, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi chake cha kupambana na ujambazi limefanikiwa kuwaua majambazi watano waliokuwa kwenye gari namba T 836 DHF aina ya Toyota Noah.

Kamanda Mambosasa ameeleza kuwa majambazi hao wapatao sita wakiwa kwenye gari hilo kwenda kufanya uhalifu maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam lakini kabla hawajatimiza lengo lao, kikosi kazi cha Jeshi la Polisi
kiliweka mtego na kufanikiwa kuzuia ujambazi huo kwa kutaka
kuwakamata wahalifu hao.

Majambazi hao walitoka kwenye gari na kuanza kukimbia huku wakiwarushia askari risasi na hatimaye askari walijibu mapigo na kufanikiwa kuwapiga risasi majambazi watano ambao walifariki dunia papo hapo na jambazi mmoja kufanikiwa kukimbia huku akifyatua risasi hovyo na kumjeruhi askari mmoja.

Baada ya kuwapekua majambazi hao walikutwa na bastola moja ikiwa na risasi tatu ndani ya Magazine na maganda mawili ya bastola.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limewatia mbaroni watuhumiwa kumi kwa tuhuma za wizi wa pikipiki ambapo wamepatikana na pikipiki 16 kufuatia operesheni iliyofanywa na jeshi hilo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wahanga wa matukio hayo ambayo yanatajwa kukithiri katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.

Jeshi la Polisi kanda Maalum Dar es salaam linaendelea na oparesheni na misako dhidi ya wizi wa pikipiki, magari na wahalifu wa makosa mengine.

Trump aendelelea kusisitiza atagombea Urais
Breaking news: Mrithi wa Maalim Seif atangazwa