Mashabiki wa Chelsea wamesisitiza msimu huu hawana bahati baada ya nyota wa timu hiyo, Cole Palmer kuumia akiwa katika majukumu ya kimataifa.
Chelsea ilimsajili nyota huyo kwa Pauni 42.5 milioni kutoka Manchester City katika dirisha la usajili la kiangazi, na alikuwa anakiwakilisha kikosi cha vijana cha England wenye umri wa miaka 20 dhidi ya Serbia, juzi Ahamis (Oktoba 12), lakini alishindwa kuendelea na mechi baada ya kuumia.
Licha ya Palmer kuumia England ilibuka na ushindi wa mabao 9-1 katika mechi ya kufuzu Euro 2024 kwa vijana.
Palmer alilazimika kutolewa uwanjani dakika ya 52 baada ya kuumia, lakini mashabiki wa Chelsea walilalamika kupitia mtandao wa X miongoni mwao wakidai hawana bahati.
Shabiki wa kwanza aliandika: “Hii ni nini? mwingine akasema: “Hakika tumelaaniwa kabisa.”
Shabiki wa tatu akasema: “Hiyo ndiyo Chelsea yetu. Tumelaaniwa au nini?”
Palmer mwenye umri wa miaka 21, ameonyesha kiwango bora tangu alipotua Chelsea kutoka Man City dirisha la kiangazi na alifunga bao na asisti mbili katika mechi tatu za mwisho.
Kocha wa timu hiyo, Mauricio Pochettino amefurahishwa na kiwango cha nyota mwingine, Noni Madueke aliyefunga bao katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Burnley.
Madueke alicheza mechi tatu tu za Ligi Kuu England akitokea benchi kutokana na majeraha.
Nyota wengine majeruhi Chelsea ni Christopher Nkunku, Romeo Lavia, Ben Chilwell, Malang Sarr, Reece James na Wesley Fofana.