Mpango wa mabosi wa Arsenal wa kumuuza kiungo wao raia wa Ghana, Thomas Partey kwenda Juventus au Saudi Arabia dirisha lijalo la usajili huenda ukafeli kutokana na majeraha yanayomsumbua fundi huyo kwa sasa.
Partey mkataba wake unamalizika mwaka 2025 na Arsenal ilipanga kumuuza ingawa kwa sasa majeraha yamekwamisha dili hilo.
Juventus ilipanga kumnunua nyota huyu ili akawe mbadala wa Paul Pogba ambaye atakosekana kwa muda mrefu kutokana na kesi yake na ilitegemewa Arsenal ingefanya biashara mapema lakini majeraha yasiyopona ya Partey yamechelewesha mipango hiyo.
Kocha wa Arsenal Mikel Arteta anadaiwa kutaka kuachana na fundi huyo kwa sababu muda mwingi amekuwa hamtumii kutokana na majeraha ya mara kwa mara anayokumbana nayo.
Awali fundi huyu alikuwa akihusishwa kuwa huenda angetimkia Saudi Arabia lakini mwenyewe inadaiwa anataka kuendelea kucheza soka la ushindani.
Tangu kuanza kwa msimu huu Partey amecheza mechi tano za michuano yote.