Majeruhi wengine 6 kati ya 38 wa ajali ya Lori iiyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro waliokuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo wakati wakiendelea kupatiwa matibabu.

Taarifa hiyo imetolewa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano na huduma kwa wateja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa maiti zote zimehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti wakati wakisubiri taratibu zingine kufuatwa.

Amesema kuwa majeruhi wengine 17 akiwemo mtoto mmoja hali zao ni mbaya na wapo katika chumba maalum cha uangalizi (ICU).

Aidha, amesema kuwa kwasasa katika hospitali ya Muhimbili wamebaki na majeruhi 32 ambao wanaendelea kuwapatia matibabu.

”Jana tulikuwa na majeruhi 38 lakini kwa bahati mbaya usiku wa kuamkia leo, majeruhi 6 wamefariki dunia kwa hiyo tumebaki na wagonjwa 32, na katika 32 hao waliobaki 17 wapo Chumba maalum cha uangalizi (ICU),” amesema Aligaesha

Hata hivyo, Aligaeshi ameongeza kuwa wanajitahidi kwa kila namna kutoa kila aina ya utaalam ili kuhakikisha majeruhi hao wanapona na kurudi katika hali zao za kawaida.

Serikali yanunua kliniki zinazotembea kusaidia majeruhi wa ajali
Watumiaji wa mabasi ya Mwendokasi DART wakwama