Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ameyataka majeshi yote nchini kuwekeza kwenye sekta ya TEHAMA ili kupambana na makosa ya kimtandao.
Ameyasema hayo leo Februari 21, jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo ya Mtandao (cybercrime) kwa Wapelelezi na Askari wa chumba cha mashtaka (CRO) yatakayodumu kwa siku tano.
Pamoja na hayo amewataka jeshi la Polisi kutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi juu ya matumizi mazuri ya mtandao na kufahamu kuhusu ni makosa gani yatamsababishia kuingia katika kosa la mtandao.
Ameongeza kuwa swala la mawasiliano kwa Majeshi yote nchini ni jambo la kuwekewa uwekezaji mkubwa ili kuwasaidia kujiandaa vizuri katika kudhibiti makosa ya mtandao na uahalifu wa aina hiyo kwa ujumla.
Aidha akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini Deusdedit Nsimeki amesema lengo kubwa la haya mafunzo ni kuwajengea uwezo askari hao ili kutambua aina ya makosa ya Jinai.
Naye Kamishina wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi Cp Shabani Hiki wa Jeshi la Polisi amewataka Askari hao kutumia mafunzo hayo katika kuleta matokeo mazuri kwa jamii na mabadiliko ili kuleta taswira nzuri kwa jeshi la polisi.