Waziri wa maji Jumaa Aweso amesema hali bado si shwari baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kutangaza mgawo wa maji
Waziri Aweso amsema hayo alipotembelea mradi wa visima saba wa Kimbiji ambao unatarajiwa kumaliza changamoto ya maji katika wilaya ya Kigamboni.
“Mara ya kwanza mtambo wa Ruvu chini pampu zetu zilikuwa hazifanyi kazi kwa sababu maji yalikuwa chini kabisa, bado hatuko stable….” amesema Aweso
“Baada ya kufanyika zile operesheni za kuwaondoa wachepusha maji, zimesaidia yale maji kuingia kwenye mkondo wa mto Ruvu na kutupa nguvu kidogo kwa maana zile pampu ziweze kujiendesha ili watu waweze kupata huduma ya maji.
“Kwahiyo bado nasisitiza hatuko stable ndiyo maana nasisitiza wananchi kile kidogo tunachokizalisha kinatumika vizuri na tunakihifadhi ili tuweze kuvuka salama,”.amesema Aweso
Aidha Waziri Aweso, amewataka Dawasa kuhakikisha ratiba za mgao zinazingatiwa na zinawekwa wazi kuhakikisha wakazi wote wa Dar wanapata maji.
“Utaratibu wa ugawaji maji uwe wazi, kama jumatatu wanapata maji Kigamboni basi wapate, kama Jumanne Sinza iwe hivyo.
“Kingine niwaombe Dawasa visima vyote vilivyochimbwa pembezoni na katikati ya mji viwe standby, vijulikane ili tujipange zaidi vituwezeshe kuvuka salama,” amesema Aweso.