Watu 32 wamepoteza maisha baada ya ukuta wa bwawa la maji kubomoka na kusababisha maji kuvamia makazi ya watu katika mji wa Solai nchini Kenya.
Tukio hilo lililotokea Jumatano usiku, kilometa 190 kutoka jiji la Nairobi, limeripotiwa kuchukua idadi hiyo ya watu wakiwemo wanawake na watoto walionasa kwenye tope.
Kitengo cha Msalaba Mwekundu nchini Kenya kimeeleza kuwa kimewaokoa watu 40 huku zaidi ya watu 2000 wakidaiwa kukosa makazi. Familia zaidi ya 450 zinahitaji mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.
Mkuu wa Polisi wa Nakuru, Gideon Kibunjah amethibitisha kuwa miili 32 imepatikana na kwamba kati ya miili hiyo, miili 11 ilikutwa katika mashamba ya kahawa ikiwa imezungushwa na tope zito.
Mmoja wa manusura wa tukio hilo, Pius Mzee alisema kuwa alikuwa anakula chakula cha usiku na wanae pamoja na mkewe, ghafla wakavamiwa na maji mengi.
Ameiambia ‘Nation’ kuwa walijaribu kukimbia lakini walishindwa kujinusuru wote, akipoteza watoto wake wawili.
“Mke wangu alikuwa na watoto wawili na mara moja ikatokea, sikuwaona. Hadi sasa sijui wako wapi’’ , alisema Pius akiwa hospitalini mjini Nakuru.
Maji yaliyotoka kwenye bwawa hilo yalisomba shule ya msingi kabla ya kusomba pia nyumba za watu na kuharibu miundombinu.
Mashuhuda wanasema kuwa usiku huo walisikia mlio mkubwa wa kupasuka kwa ukuta na baadaye walishtushwa na maji mengi yaliyowavamia.