Mganga Mku wa Serikali, Prof. Abel Makubi ameuagiza Uongozi wa Maabara ya taifa ya Afya ya Jamii kutoa majibu ya sampuli za Ugonjwa wa Covid-19 ndani ya saa 24, badala ya saa 72 kwa hospitali zinazopeleka Sampuli hizo, au kwa wananchi wanaojitokeza kupima ugonjwa huo kwa nia ya kutaka kusafiri nje ya nchi.
Prof. Makubi ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na Uongozi wa Maabara hiyo, Waganga wakuu na wasimamizi wa Maabara kutoka Hospital za Rufaa za Serikali na za Binafsi kutoka mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kufanya ziara katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya jamii, kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili maabara hiyo.
Amesema lengo ni kuondokana na malalamiko ambayo yamekuwa yakielekezwa kwa maabara hiyo kuwa kuna ucheleweshaji mkubwa wa majibu ya vipimo hivyo.
Prof. Makubi amesema pamoja na kuweka mifumo mizuri katika maabara hiyo lakini bado kumekuwepo na malalamiko wanayapokea kutoka kwenye baadhi ya Hospitali na hata kwa wasafiri wanaofika katika maabara hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, ucheleweshaji ambao umekuwa kero kwa wananchi hao.
“Tafuteni njia mtakayofanya ila hakikisheni kuanzia sasa majibu yote ya Covid-19 yanatolewa ndani ya saa 24 kwa wale wote watakaofanyiwa vipimo kwa Dar es salam na masaa 48 kwa mikoani, na lazima suala hili lisimamiwe na wasimamizi wote wa maabara zinazohusika ili kuhakikisha kero hii inaondolewa,” amesema Prof. Makubi.