Ripoti ya kila mwaka ya Siku ya UKIMWI Duniani ya Shirika la kupambana na UKIMWI la Umoja wa Mataifa – UNAIDS, imeeleza kuwa majibu ya maradhi hayo yanayotolewa na jamii yamekuwa hayatambuliki, hayafadhiliwi ipasavyo na katika baadhi ya maeneo yanashambuliwa.
Ripoti hiyo inakuja ambapo tayari Umoja wa Mataifa ukiwa umeweka lengo la kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo 2030, huku watu milioni 39 duniani kote wanaoishi na VVU, milioni 20.8 kati yao wako mashariki na kusini mwa Afrika na milioni 6.5 wako Asia na Pasifiki.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa kati ya watu milioni 39, milioni 9.2 hawana matibabu ya kuokoa maisha yao na ujumbe wa ripoti hiyo unaonesha matumaini makubwa licha ya Dunia kwa sasa ikiwa inapambana kukomesha UKIMWI kama tishio la afya ya umma.
UNAIDS ilisema, “sheria na sera zenye madhara kwa watu walio katika hatari ya kuambukizwa VVU, ikiwa ni pamoja na watu wanaofanya biashara ya ngono, watu waliobadili jinsia na watu wanaotumia dawa za kulevya ni tishio lililopo.”