Uongozi wa Namungo FC umefikia makubaliano na kunasa saini ya winga mshambuliaji, Hamad Majimengi kwa mkataba wa miaka miwili.
Nyota huyo aliyeachana na Coastal Union baada ya kumaliza mkataba, awali ilielezwa alisaini pia KMC, lakini taarifa zinaeleza kuwa ameikacha timu hiyo na kujiunga na Namungo FC.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Namungo FC, Omar Kaaya amesema bado wanaendelea na usajili na watakapokamilisha wataweka wazi.
“Kuna wachezaji ambao bado tuko kwenye mazungumzo nao na nisingependa kuwaweka wazi kwa sasa hadi pale tutakapofikia makubaliano rasmi, mashabiki zetu watambue tutasajili wachezaji bora watakaokidhi matakwa ya benchi la ufundi,” amesema Kaaya.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi amesema moja ya mapendekezo yake kwa viongozi ni kupatiwa winga wenye uwezo, jambo ambalo mabosi wa timu hiyo tayari wamelifanyia kazi baada ya kuondoka kwa Kassim Haruna ‘Tiote’ aliyevunja mkataba.
Katika mapendekezo mengine ya Kitambi ni eneo la ushambuliaji akihitaji mshambuliaji mwingine atakayesaidiana na Reliants Lusajo.
Mbali na Majimengi wengine waliotua Namungo FC iliyoweka kambi jijini Arusha ni kiungo mkongwe Erasto Nyoni aliyejiunga akitokea Simba SC iliyompa ‘Thank You’.