Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limetaja majina ya watuhumiwa sugu wanaopora wananchi kwa kutumia pikipiki katikati ya jiji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Kaimu kamanda wa polisi kanda maalum, Kamisha msaidizi wa polisi (DCP) Lucas Mkondya, amesema jumla ya watuhumiwa 10 walikamatwa katika operesheni ya kudhibiti uhalifu na kuwataja viongozi wao.
Amesema viongozi wa uhalifu huo ni Carlos Thobias (18), Boniface George (20), Akida Twaha (21) na Deogratius Lyamuya (26) wote wakiwa wakazi wa Kimara. “Tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 10 wanaojihusisha na uhalifu katika maeneo mbalimbali na kuwataja wenzao wengine 13 ambao wanajihusisha na uporaji kwa njia ya pikipiki”, amesema Mkodya.
Amesema watuhumiwa wote walikiri kuhusika pamoja na kushiriki matukio ya kupora wananchi vitu mbalimbali ikiwemo simu, televisheni na laptop.
“Watuhumiwa hawa wanafanya uhalifu maeneo ya Kimara, Sinza, Magomeni, Kawe na katikati ya jiji na kuwakaba watu huku wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki, tumewakuta na televisheni 1, laptop 1 na simu 9 za aina tofauti”, alisema Kamanda Mkodya.
Aidha, Jeshi hilo limekamata jumla ya watuhumiwa 275 kwa makosa mbalimbali ya kiuhalifu pamoja na dawa za kulevya kwa kipindi cha wiki moja. Amesema makosa hayo ni pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha, utapeli, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kuuza pombe haramu na kupatikana kwa bangi katika maeneo mbalimbali ya jiji.
“Operesheni hii ni endelevu jumla ya kete 96 za dawa za kulevya tumezikamata, puli 156, misokoto ya bangi 86, magunia 15 ya bangi pamoja na pombe na gongo ipatayo lita 60”, amesema Mkondya.
Pia, Jeshi hilo litaanza operesheni maalum ya kudhibiti wapiga debe katika vituo mbalimbali vya daladala kuanzia Agosti 14 mwaka huu.
“Kuanzia Jumatatu hatutaki wapiga debe katika vituo vyote vya mabasi kwa sababu wahalifu wengine hutumia fursa hiyo kufanya uhalifu hasa nyakati za usiku, nasisitiza ni marufuku kuwepo kwa wapiga debe katika kituo chochote cha daladala”, ameongeza Mkondya.
Katika hatua nyingine Jeshi la polisi kupitia kikosi cha usalama Barabani limefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 463 kwa kipindi cha wiki moja ikiwa ni tozo za makosa ya usalama barabarani kanda ya Dar es salaam.