Mkurugenzi mtendaji wa E Media Group Francis Ciza maarufu Majizzo amatoa mtazamo wake juu ya tuzo za muziki Tanzania na kuwakosoa wasanii kadhaa waliozibeza na baadhi kujitoa katika ushiriki wa tuzo hizo.
Majizo ameyasema hayo kwa njia ya maandishi aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ikiwa ni siku moja pekee imesalia kuelekea kilele cha utolewaji wa tuzo za muziki Jumamosi Aprili 2 mwaka 2022.
Majizzo ameweka wazi kuwa uwepo wa tuzo kwenye tasnia ya muziki ni jambo la muhimu, na zina mchango kwenye tasnia ambao ulionekana kwa kiwango kikubwa wakati wa Tuzo za Kilimanjaro ambazo zilipotea kwa kipindi kirefu.
“Tuliokaa kwenye hii game kwa miaka mingi tunafahamu jinsi ambavyo watu walihangaika kuja na tuzo, ‘Kili Music Award’ zilikuwa tuzo zetu kubwa zaidi, na japo zilikuwa na madhaifu mengi lakini atakuwa mtu wa hovyo sana atakayeshindwa kutambua mchango wa tuzo zile kwenye muziki wetu, alisema Majizzo.
Majizzo ameongeza kuwa hatotaka kutaja majina ya wasanii ambao walivuma wakati wa tuzo hizo na wengine kupata tuzo nyingi.
“Hazikuwa tuzo za Kimataifa, ni za HAPA NDANI. Angalau kumbukeni jinsi ambavyo tuzo zilichangamsha game na kufanya watu watoe kazi kali sana,” ameongeza.
“Baada ya muda mrefu wa sisi kutamani tuzo, Serikali yetu sikivu chini ya Wizara inayosimamia Sanaa imetuletea Tuzo za Muziki Tanzania. Ni kichekesho cha mwaka kusikia kuna wasanii wametukana tuzo hizi na kusema sio lolote. Wamebeza jitihada hizi za Serikali na wadau wengine wa Muziki,” ameongeza.
Hata hivyo amewataka wasanii kuacha tabia ya ubinafsi na kuona hazikua na msaada akiongeza kuwa ni tuzo zilizowainua wasanii wnegi na kujenga majina yao.
“Ni kweli zina madhaifu, kama ambavyo tuzo zote Duniani hupata malalamiko, sio ajabu hizi zetu kulalamikiwa, Lakini mnapojitoa kwenye tuzo au mnapogomea tuzo na kuzikejeli, wazeni faida ambazo hizi tuzo zinaweza kuleta. Wazeni kuhusu wasanii ambao zitawajenga, wazeni kuhusu wengi ambao tuzo hizi zitakuwa sherehe kwao na chachu ya wao kutengeneza kazi bora zaidi. Kwa kufanya hivyo mtaisidia ‘Industry’, kabla ya kusema tunawaza tuzo za Kimataifa, tuzipe heshima za kwetu, tuwaze pia kundi kubwa la wanamuziki ambao bado wanahitaji hizi tuzo,” aliandika Majizzo.
Hata hivyo ameishukuru Wizara inayosimamia sanaa, na Waziri mwenye dhamana, Katibu Mkuu na watendaji wote wa sanaa kwa kuanzisha tena Tuzi hizo akiwaomba kuangalia makosa na kuyarekebisha kwa kushirikiana na wasanii.
“Pongezi wasanii wote walioshiriki. Mshinde au msishinde ninyi ni Washindi.” amewapongeza Majizzo.
Mkongwe huyo kwenye tasnia ya Muziki Tanzania anewataka wasanii kuzidi kushirikiana katika kuupa nguvu muziki, kuzipa nguvu tuzo na mengine yote yenye faida kwa muziki wa Tanzania akitumia usemi wa ‘kuacha roho za korosho’.