WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuitangaza kwa bidii filamu ya Royal Tour pamoja na vivutio mbalimbali vilivyoko nchini.
“Ninawasihi Watanzania tusishawishike kudharau vya kwetu, tusimame pamoja kutangaza vivutio vyetu na kupitia utalii huu, tutafungua ajira kwa waongoza utalii na kada nyinginezo,” amesema.
Ametoa wito huo leo usiku (Jumapili, Mei 15, 2022) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali na mamia ya wakazi wa mkoa wa Dodoma waliofika kushuhudia uzinduzi wa filamu hiyo, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
“Baada ya hapa, wana Dodoma twende tukaisemee filamu hii kwa kutumia simu zetu na mitandao ya kijamii,” amesema Waziri Mkuu ambaye alikuwa akimwakilisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.
Amesema kuzinduliwa kwa filamu ya Royal Tour kumefungua zaidi milango ya utalii na kwani baada tu ya uzinduzi Tanzania ilipokea watalii 796 kutoka Israeli ambao walikuja kwa ndege tatu zilizofuatana.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka Wakuu wengine wa Mikoa watenge siku moja na kuwashirikisha wananchi wao washuhudie kazi kubwa ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais.
“Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Mtaka yeye kaanza. Ni vema Wakuu wengine wa Mikoa watafute siku moja ya kuwaonesha watu wao, wanaweza kuchagua hata kwenye ngazi ya Halmashauri ili waone juhudi za Mheshimiwa Rais wetu,” amesisitiza.
Amesema kitendo cha Mheshimiwa Rais Samia kuruka kwa ndege na kuonesha kwa karibu kilele cha Mlima Kilimanjaro, kimekata mzizi wa fitna juu ya mahali halisi ulipo mlima huo. “Mheshimiwa Rais amekata mzizi wa fitina na kuithibitishia dunia kuwa Mlima Kilimanjaro uko Tanzania.”