Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, umedhamiria kuiboresha safu ya ushambuliaji, baada ya kuona mapungufu katika michezo ya Ngao ya Jamii, na shabaha kuu imeelekezwa kwa Mshambuliaji kutoka DR Congo na Klabu ya Al Hilal ya Sudan, Glody Makabi Lilepo.
Awali Young Africans ilifanya mazungumzo na Mshambuiajı huyo, ambaye walitaka kumsajili katika usajili huu ili kuchukua nafasi ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika, Fiston Mayele aliyetimkia Pyramids FC ya Misri.
Young Africans ilishindwa kufikia muafaka mzuri na uongozi wa Al Hilal kwa ajili ya kumsajili Lilepo, kabla ya kuhamishia Konkoni aliyetambulisha nguvu kwa Mghana, Hafizi hivi karibuni.
Mmoja wa mabosi wa Young Africans, amesema kuwa, uongozi wa timu hiyo umekubali kuvunja benki na kumtengea Lilepo kitita kikubwa cha dau la usajili ili akubali kusaini mkataba wa miaka miwili aliowekewa mezani.
Bosi huyo amesema Mshambuliaji huyo hivi sasa ameondoka katika kambi ya Al Hilal kama sehemu ya kushinikiza aruhusiwe kuondoka klabuni hapo kabla ya dirisha la usajili kufngwa Agosti 31, mwaka huu.
Aliongeza kuwa, Mshambuliaji huyo yupo katika mazungumzo na mabosi hao wa Young Africans, na kama yakienda vizuri, basi atasaini.
“Uongozi umeangalia kikosi chetu katika mashindano ya Ngao ya Jamii na kugundua upungufu mkubwa katika safu ya ushambuliaji ambayo ni lazima wampate mshambuliaji wa kiwango kikubwa zaidi ya hao waliokuwepo sasa.”
“Lilepo ni kati ya washambuliaji watakaosajiliwa kabla ya dirisha kufungwa msimu huu, kwani ni mchezaji aliyekuwepo katika mazungumzo mazuri na Uongozi baada ya yeye mwenyewe kuhitaji kuja Young Africans.”
“Tayari mshambuliaji huyo ameondoka kambini huko Al Hilal akishinikiza kuvunjwa kwa mkataba wake, hivi sasa yupo katika mazungumzo mazuri na vongozi wake na kama yakienda vizuri, basi huenda akasaini Young Africans kabla usajili haujafungwa,” amesema bosi huyo.
Makamu wa Rais wa Young Africans, Arafat Haji, hivi karibuni katika Wiki ya Wananchi, alizungumzia usajili na kusema kuwa: “Bado hatujafunga usajili wetu wa msimu huu, hivyo tunaweza kuongeza wachezaji mmoja hadi wawili kabla ya dirisha kufungwa.”