Umoja wa Mataifa umeonesha uwepo wa hali ya kitisho nchini Libya baada ya taarifa zilizobaini uwepo wa makaburi manane ya watu wengi, katika eneo ambalo liliweza kudhibitiwa na serikali ya kitaifa kufuatia wapiganaji wa mbabe wa kivita Khalifa Haftar kuondoka katika eneo hilo.
Taarifa ya mpango wa ulinzi wa amani nchini Libya (UNSMIL) inasema makaburi hayo yamebanika katika eneo la Tarhuna, kusini mashariki mwa mji mkuu Tripoli, siku chache zilizopita.
DW wameripoti kuwa taarifa hiyo imeongeza kwa kusema “sheria ya kimataifa inaitaka mamlaka kufanya uchunguzi madhubuti na wa haraka, wenye uwazi ili kuwafikisha katika mikono ya sheria wale wote waliohusika na mauwaji”.
Mwandishi wa shirika la habari la Ufaransa AFP alipata nafasi ya kufika katika eneo ambalo miili kadhaa ya watu ilifukuliwa na Shirika la Hilali Nyekundu kwa ajili ya utambuzi.