Makada 15 wa Chadema waliojitambulisha kuwa viongozi wa chama hicho Wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza wamehama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Makada hao wakiongozwa na Damas Kimenyi aliyejitambulisha kuwa Katibu Chadema wa Wilaya hiyo walitaja kuridhishwa na utendaji wa Rais John Magufuli na mbunge wa jimbo la Ilemela, Angelina Mabula kuwa miongoni mwa sababu za kujiunga na CCM.
Wanachama hao wapya wamepokelewa katika ofisi za CCM Wilaya ya Ilemela wakati wa hafla iliyoongozwa na Mwenyekiti wa wilaya hiyo, Nelson Mesha.
Hata hivyo, Katibu Chadema Kanda ya Ziwa, Meshack Micus amesema waliohamia CCM walishavuliwa uongozi tangu Januari 18, mwaka huu wakati wa kikao cha Mkutano Mkuu wa Wilaya ambacho pia kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe.
“Hao ni wanachama wa kawaida na pengine wameondoka kwa hasira ya kuvuliwa madaraka baada ya Mkutano Mkuu kuunda kamati ya muda ya uongozi chini ya uenyekiti wa Warioba Wanzagi na Katibu wake Peter Kaiza,” amesema Micus.
Wengine waliojiunga na CCM ni Lukas Syrilo (Katibu wa Baraza la Vijana Bavicha), Agnes Majora (Katibu wa Baraza la Wanawake, Bawacha), Lucy Kazungu (Mwenyekiti Bawacha), na Edwine Sarungi aliyejitambulisha kuwa Mweka Hazina.
Pia wamo Philipo Richard Mjumbe wa kamati tendaji wa Wilaya, Ester Ayoub Makamu Mwenyekiti wa wazee Wilaya, John Haule Mwenyekiti Bavicha, Vestina Johnson Mjumbe wa Bawacha Wilaya na Yohana Emanuel Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa wilaya