Na Josefly:
‘Dawa ya jeuri ni kiburi’. Huu ni msemo maarufu wa Kiswahili wenye maana kubwa. Na kiburi hunoga hasa pale unapogundua anayekufanyia jeuri anajua fika kuwa una gunia la almasi iliyolowa tope. Kwahiyo, anachofanya ni kuhakikisha hauisafishi ionekane mbele ya watu. Wakati mwingine, ni wivu tu!
Julai 6, 2004, Rais wa Pili wa Msumbiji, Joaquim Chissano ambaye wakati huo alikuwa na kofia ya Uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), aliishangaza dunia na wale wajeuri wenye lugha zao. Aliamua kutumia lugha ya Kiswahili kutoa hotuba yake muhimu sana ya kuaga akimuachia kijiti cha uenyekiti Rais wa Nigeria wa wakati huo, Olusegun Obasanjo.
Chissano aliamua kama ‘mbuayi na iwe mbuayi’. Uamuzi wake ulitokana na jinsi ambavyo ombi la kurasimisha lugha ya Kiswahili kuwa moja kati ya lugha rasmi za AU lilivyokuwa linapigwa danadana. Wakati huo, lugha rasmi zilizotambulika katika mikutano ya AU zilikuwa ni Kiarabu, Kireno, Kiingereza na Kifaransa. Yaani lugha tatu za mabeberu walioitawala Afrika, ndizo zilikuwa zinatawala mikutano ya Afrika Huru pamoja na Kiarabu!
Mzee Chissano akachapa Kiswahili mwanzo-mwisho. Wale wajeuri wakahamaki, yeye akaendelea tu. Wakaomba poo! Akawaambia ruksa kutumia mkalimani, wakavaa ‘headphone’ wakamsikiliza mkalimani kwa lugha zao, wakampambana na hali zao siku hiyo. Ndiyo, wajifunze Kiswahili, lugha yenye alama ya Uafrika.
‘Kiburi’ kile kilizaa matunda ya aina yake. Wenye jeuri wakanyoosha mikono. Kumbuka Mzee Chissano hata Kiswahili kwake hakikuwa lugha ya kwanza au lugha ya taifa lake, alijifunza tu. Aliona hii ni almasi ndani ya tope, akaimwaga mbele ya umati na akaisafisha kwelikweli, kila mtu akaiona na kuanza kuihangaikia. Mabeberu wakaandika mengi kuponda kuwa haikuwa sawa mbele ya mkutano wa wengi wasioelewa Kiswahili, lakini walishindwa wakalegea.
Sasa kila mtu akajaribu kuvutia kwake. Balozi wa Sudan nchini Ethiopia wakati huo, alimkaribisha Mzee Obasanjo aliyekuwa anachukua nafasi ya Uenyekiti, akasema atazungumza Kiarabu kwakuwa nayo ni lugha ya Kiafrika. Kumbuka Sudan wanazungumza Kiarabu. Ni sawa, kwa sababu Kiswahili chenyewe kimekopa maneno mengi kutoka kwenye lugha ya Kiarabu. Hata neno ‘Swahili’ lilitumiwa na Waarabu wa zamani kumaanisha ‘Pwani’.
Kiswahili kina mtaji wa watumiaji zaidi ya milioni 135, na zaidi ya milioni 5 kwao ni lugha ya kwanza (kilugha). Ingawa kilizaliwa Pwani ya Afrika Mashariki, tunakubaliana kwamba nyumbani kwao ni Tanzania.
Hivi sasa nchi takribani tano zimepitisha lugha hii adhimu kuwa lugha yao ya Taifa. Nchi hizo ni pamoja na Kenya, Uganda, Namibia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wameona jinsi lugha hii ilivyowaunganisha Watanzania na kuondoa ukabila, kudumisha amani na umoja. Ni lugha ya ukombozi wa Bara la Afrika.
Lakini, Watanzania sijui nani alikuwa ametuloga! Wiki tatu zilizopita, Kenya ilitupiga kanzu, ikasaini makubaliano maalum (MoU) kufundisha Kiswahili nchini Afrika Kusini. Tunaambiwa Bondeni kwa Madiba kuna fursa, 40% ya wanaosoma huko wanazungumza Kiswahili. Zaidi, Serikali ya nchi hiyo imepitisha Kiswahili kifundishwe kila ngazi ya elimu.
Tukajiuliza, kwani Wakenya wanajua Kiswahili kuliko sisi? Hapa tutawabishia hadi mwisho. Sasa Watanzania nani atatutoa tongotongo, tuone mbele tukajitwalie fursa yetu? Lakini wapo walimu wengi tu wa Kenya wanaofundisha Kiswahili kwenye vyuo vyetu, utashangaa na hili.
Dunia inatafuta almasi tuliyonayo sebuleni. Jirani mwenye makapi ya almasi anatufunga magoli sokoni. Tunakwama wapi???
Walimu wanakosaje ajira wakati dunia inawasaka wafundishe lugha tunayojidai nayo, tena tusiyoithamini sana ndani! Huku kwetu ukiongea kizungu ndio unaonekana msomi, wakati hata wazungu wanakisaka Kiswahili. Wamemwagika vyuoni wanajifunza lugha yetu, sisi tunatukuza yao!
Hata hivyo, kwa bahati nzuri, aliyetuloga Watanzania hakubahatika kutuloga wote.
Wiki iliyopita, Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli aliilipiza kanzu tuliyopigwa na Wakenya kwa kufunga magoli kumi kwa tikitaka. Akiwa kwenye hafla za kumuapisha Rais Cyril Ramaphosa, Rais Magufuli alifanikiwa kumshawishi Rais huyo kuwa lile soko la Kiswahili nchini humo tuingie wajuzi wa lugha yetu, Waswahili wenyewe. Ikafungwa dili. Sasa maelfu ya Watanzania watakuwa wanaingia Bondeni sio kuzamia kutafuta maisha kwa njia za panya, ni kwenda kupiga kazi ya kuwafunza lugha yetu adhimu mamilioni wenye kiu ya kuifahamu.
Nikajiuliza lakini Watanzania tumejipanga vipi kulilisha vizuri soko hili ili tuwafunike wenzetu kwa almasi safi zaidi ya Kiswahili? Majibu niliyapata juzi nikiwa kwenye mahafali ya 49 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kati ya wahitimu 49 wa Shahada za Udaktari wa Filosofia (PhD), 10 wamehitimu kwenye Kiswahili. Yaani PhD 10 za lugha ya Kiswahili. Nikaamini, kweli majembe ya Kiswahili yapo.
Kati ya wahitimu wote, hawa 10 ndiyo waliokuwa wanapigiwa shangwe kuu zaidi. Na hawa pekee ndio waliomfanya Mkuu wa Chuo, Dkt. Jakaya Kikwete (Rais Mstaafu), kufunguka:
“Nyie ndiyo mna uhakika wa soko kubwa la ajira kimataifa. [Soko) linawasubiri, hongereni sana.”
Dkt. Kikwete ameiona fursa duniani, anawaona wanaoenda kufaidi, soko linawasubiri. Rais Magufuli kafungua mlango tushuke Bondeni kwa Madiba. Sasa, Wizara husika na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) tusiangushane jamani. Tumetafuniwa… tusishindwe kumeza tu!
Ni wakati wa kuhakikisha tunaisafisha hii almasi yetu (Kiswahili), tukaiuze kwa bei ya juu na kupandisha uchumi wetu. Tutatafsiri vitabu, tutakuwa wakalimani, tutauza kazi zetu za sanaa kirahisi duniani, tutawavutia watalii. Wasomi, angalieni soko hili hapa la kimataifa, someni Kiswahili.
Rafiki yangu mmoja anaitwa Sarah, mimi humuita Swahiba, yeye amekuwa akipiga pesa tangu mwaka 2015, anafundisha Kiswahili wazungu wachache tu tena nyumbani kwake. Angalau wajue salamu na mambo ya msingi (basics). Ila anachoingiza kwa mwezi ni ‘vimilioni kadhaa’.
Kiswahili ni noma, ni dili. Ni almasi mchangani iokote, isafishe ikupe maisha.
Ila nikutahadharishe tu, achana na Kiswahili kilichochakachuliwa mtaani. Kiswahili sio rahisi sana, ingia darasani soma, jifue, tembelea kamusi za Tuki. Kama unabisha, niambie ‘Of course’ kwa Kiswahili fasaha. Je, ufahamu maana ya tashtiti au tasnifu? Usichukulie poa, Kiswahili fasaha sio Kiswazi.