Tatizo la wizi wa mifugo Wilayani Rorya mkoani Mara limekuwa likijitokeza kila mara, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wananchi kujikuta katika umaskini baada ya kuibiwa mifugo yao
 
Kuendelea kuwepo kwa wizi wa mifugo baadhi ya Madiwani kutoka Kata 14 wakiwemo wa chama cha Mapinduzi CCM na Chama cha Democrasia na Maendeleo Chadema kutoka Wilaya ya Rorya na Tarime wakaamua kuungana kwa pamoja kufanya mkutano wa ujirani Mwema uliokuwa ufanyike Machi 28-2019 katika Kijiji cha Kitembe Kata ya Kitembe Wilayani Rorya ili kujadili na Wananchi namna gani watakomesha wizi pamoja nakupanga mikakati mipya lakini haukufanyika.
 
Wananchi na Madiwani wakiwa wamewasili kwenye mkutano huo ghafla Diwani wa Kata hiyo ya Kitembe, Thomas Patrick (Chadema) akawaeleza Madiwani na Wananchi kuwa amepigiwa simu na Afisa Tarafa ya Girango, Jamsi Chambiri kuwa Mkuu wa wilaya ya Rorya, Simon Chacha amezuia kufanyika kwa mkutano huo na kuagiza kila Diwani akafanye mkutano kwenye Kata yake na akaamuru Madiwani kuondoka mara moja na kutozungumza chochote na hivyo Madiwani wakalazimika kuondoka.
 
“Wananchi na Madiwani mlioshiriki mkutano kwa nia ya kutafuta suluhu juu ya wizi wa mifugo unaokabili kata zetu nawashukuru kwa kuhudhulia lakini niwaombe radhi nimepigiwa simu na Afisa Tarafa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya amesema tusifanye mkutano nakwamba Madiwani wasijadili chochote na waondoke eneo la mkutano kwakuwa si kata yao hawapaswi kushiriki kwa lolote” amesema Patrick.
 
Akizungumza kwa njia ya simu Afisa Tarafa huyo ameeleza kuwa” ni agizo la Mkuu wa wilaya amesema Diwani wa Kata ya Kitembe anatakiwa mwenyewe ndiyo afanye mkutano kwakuwa ni Kata yake hao Madiwani wengine hawapaswi kufanya mkutano, hivyo wakafanye mkutano kwenye kata zao, istoshe Rais alizuia mikutano akasema kila mtu afanye mkutano kwenye eneo lake nasiyo kwenda Kwenye Kata ya mwingine ama Jimbo lisilo lake,”amesema.
Kauli ya DC Rorya.
 
Akizungumza kwa njia ya simu, mkuu huyo wa wilaya anesema kuwa amezuia mkutano kwakuwa Diwani wa Kata ya Kitembe hana kibali cha Kuwaita Madiwani kutoka kata mbalimbali na kufanya nao mkutano kwenye kata yake nakwamba kama ni kufanyika kwa mkutano uwe ni wa Kata ya hiyo pekee na usiwashirikishe Madiwani wengine na akawataka Madiwani hao kwenda kufanya mikutano kwenye kata zao.
 
“Kata ya Kitembe ndiyo inaongoza kwa wizi wa mifugo Mimi sijamzuia asifanye mkutano wake isipokuwa ni marufuku kushirikisha Madiwani wengine kila Diwani akafanye mkutano kwenye kata yake hiyo kata tulishafanya mkutano Mimi mwenyewe nilishakwenda Kitembe’ Mbunge alishakwenda ,RPC na OCD walishafika na wakazungumza na wananchi wakaeleza kero zao Polisi wanazifanyia kazi” anasema Chacha.
 
Ameongeza kuwa”Diwani hana kibari cha kualika Madiwani wa Kata zingine kushiriki kwenye mkutano wake kuna taratibu za kufatwa vinginevyo mkutano huo ungekuwa umeitishwa na Mkuu wa wilaya au RPC kwa hiyo nimeuzuia usifanyike na kama ni kufanyika uwe ni wa kata ya Kitembe tuu usihusishe Madiwani wa Kata zingine,” amesema
 
Wananchi wamshangaa DC.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari wananchi wa kata ya Kitembe na wananchi kutoka kata zenye mgogoro wa wizi wa ng’ ombe wameonekana kutofurahishwa na zuio hilo la mkutano licha ya kutumia gharama za usafiri wengine kutembea umbali mrefu kushiriki mkutano ili kujadili kero za wizi wa mifugo lakini hitaji lao halikutekelezeka baada ya Madiwani waliowategemea kushirikiana pamoja kuzuiliwa kuzungumza chochote.
 
Erasto Uma mkazi wa Kitongoji cha Midamba Kijiji cha Kitembe amesema kuwa hivi karibuni aliibiwa ng’ ombe 9 “ nilivyosikia leo kuna mkutano nilifarijika sana nikasema huenda kutapatikana suluhisho, ng’ombe zetu zinaibwa kutoka Rorya zinapelekwa Wilayani Tarime kata ya Bumera zinaishia huko na zingine zinavushwa kwenda Kenya, sasa tulitegemea huu mkutano DC angeufurahia maana Madiwani kwa nia moja walikuja kutusaidia ili tutatue suala hilo lakini kazuia mkutano haukufanyika tumechukia sana” amesema Uma.
 
David Chacha ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Sombanyasoko kata ya Komaswa Wilayani Tarime amesema kuwa aliamua kushiriki mkutano huo kwa gharama zake za nauli sh.20,000 kwa usafiri wa pikipiki hadi Wilayani Rorya ili kujadiliana kwa pamoja kwakuwa Kijiji chake ng’ ombe zimekuwa zikiibwa kila mara licha ya kufanya mikutano ya kujadili wizi ndani ya Kijiji lakini wizi unaendelea.
 
“Tangu mwaka jana hadi sasa ng’ombe 300 zimeibiwa wananchi hawana amani tukaona kuna haja ya kufanya vikao vya ujirani mwema tuone tutasaidianaje maana Polisi tumekuwa tukiwapa taarifa hizi kunapotokea wizi lakini tunaendelea kuibiwa wahusika wanakamatwa na kuachiwa”amesema Chacha.
  • Maonyesho ya tafiti UDSM yaanza rasimi
 
Saimon Oguma mkazi wa Kijiji cha Sakawa amesema ni Mara yake ya sita kuibiwa ng’ombe ambao wamefikia idadi ya ng’ombe 25 na wanapofuata nyayo zinaishia Kijiji cha Bumera Wilayani Tarime hivyo alitegemea mkutano huo ungeleta matumaini kwake.
 
Nyakore Joseph mkazi wa Kijiji cha Nyambogo anaeleza kuwa iwapo mkutano huo ungefanyika zingepatikana njia za utatuzi kwakuwa uliwahusisha Madiwani wa kata mbalimbali zikiwemo kata zinazotuhumiwa kuhusika na wizi,hivyo kitendo cha Mkuu wa wilaya kuzuia kinawapa maswali mengi ya kujiuliza licha yakuwa kiongozi huyo ndiye Mwenyekiti wa ulinzi na Usalama wa wilaya lakini kazuia mkutano uliolenga kuleta utatuzi.
 
Seka Onindo ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Wang’elung’o Kijiji cha Nyambogo amesema hadi sasa zimeibwa ng’ombe 40 na hakuna ng’ombe iliyopatikana tofauti na mwezi Machi mwaka huu ziliibwa ng’ombe 9 ambapo zilifuatiliwa na wafuata nyayo na zote zikapatikana, hivyo anaiomba Serikali iwasaidie kwani wizi umewachosha usiku hawalali wakikesha kulinda, jambo ambalo limeondoa amani na furaha kwa wananchi.
 
Charles Ongili ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitembe amesema kuwa wizi wa mifugo umeleta umasikini kwa wananchi kwakuwa wanategemea ng’ombe katika Kilimo, Maziwa, Nyama, Mahari na hata kuuza ambapo hupata pesa za kusomesha watoto na mahitaji mengine na wanapotoa taarifa Serikali haiwasaidii.
 
Madiwani, Mwenyekiti wa CCM Rorya, Katibu wa Chadema Mara wamesema haukuwa mkutano wa kisiasa.
 
Kitendo hicho cha zuio la mkutano kinaelezwa kuwakera viongozi hao wa kisiasa na kudai kuwa mkutano huo haukuwa wa kisiasa bali wa kujadili na kupanga mkakati wa kutokomeza wizi wa mifugo ambao umekuwa tishio na ulihusisha Madiwani kutoka Kata 14 kati ya hizo 11 ni za Madiwani kutoka Chama cha Mapinduzi CCM kati ya hizo Tisa ni Madiwani wa CCM kutoka Rorya na 2 Madiwani wa CCM kutoka Kata zilizopo Wilayani Tarime, ambapo Kata 3 ni za Madiwani kutoka Chama cha Democrasia na maendeleo Chadema kutoka Rorya.
 
Kata hizo 14 ambazo ni Kata ya Kitembe, Nyathorogo, Rabuor Kinyenche, Mirare, Kisumwa, Roche, Kigunga, Goribe, Ikoma, Raranya na Nyahongo zote kutoka Rorya na Kata ya Komaswa na Bumera kutoka Wilayani Tarime, zinaelezwa ndizo zinakabiliwa na tatizo la wizi wa Mifugo na hivyo Madiwani kuamua kufanya mkutano wa ujirani Mwema ili kupata suluhu.
 
Diwani wa Kata ya Nyathoro, Jeremia Kan Luande (Chadema) amesema kuwa lengo la Madiwani kukutana katika mkutano ilikuwa kupokea kero za wananchi kuzijadili kisha kupanga mikakati ya pamoja namna gani watadhibiti ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa ununuaji mifugo, uuzaji na usafirishaji.
Wapinzani wasusia bunge hukumu ya Lema, watoka nje
 
“ Tulikuja na mikakati mipya watu wanaonunua mufugo lazima wajulikane kanunua wapi na kwa nani na je ana barua ya usafirishaji ili kuwa rahisi kubaini wezi wanaosafirisha ng’ombe ,kwakuwa wenyeviti wa vitongoji ndiyo wanawatambua wananchi kwa urahisi ndiyo tulitaka wawe watoaji wa barua.
 
Ameongeza kuwa ”na mtu anayepokea mifugo aone kibari cha usafirishaji kinatoka wapi na tulitaka hawa wakaguzi wa nyama na wachinjaji tuwashauri ikiwa ni pamoja na kufika kwa muda kwenye machinjio ili kujua ng’ombe hao wanatoka wapi!hili zuio limetuumiza hatukuja kisiasa ndiyo maana Madiwani tuko vyama vyote lengo kupata muafaka ili wananchi wasiumie.”amesema Luande.
 
Diwani wa Kata ya Komaswa Wilayani Tarime, Leonce Bartazar (CCM) amesema sababu ya kushiriki katika mkutano ni kutokana na uwepo wa changamoto ya wizi wa mifugo.
“Wananchi wangu wanaibiwa sana ng’ombe tulitaka kujua hao wezi wanatoka wapi na wanashirikiana na nani?maana wapo wezi wanaotoka kwenye kata yangu wanashirikiana na wa Rorya tukaona Madiwani tukutane huenda tutapata muafaka, naomba Serikali ilitazame hili maana kila wiki zaidi ya ng’ombe 50 zimeibwa kutoka kwenye Kata yangu tumefanikiwa kurudisha ng’ombe 16 pekee sasa Mimi kama Diwani lazima nitafute njia mbalimbali za kulikabili hili ili chama changu kisipate doa,”amesema.
 
Diwani wa Kata ya Bumera -Tarime Deogratias Ndege amesema” Kata yangu ya Bumera ndiyo inatuhumiwa kwa kuiba ng’ombe kutoka Rorya na nimeshaona kuna viashilia vya kuja kutokea mapigano kati ya Wajaruo na Wakurya hivyo nikaamua nami kushirikiana na Madiwani wenzangu tuone tutafanyaje nikaamua kufunga safari kutoka Musoma nimegharamika mafuta lakini nafika eti mkuu wa wilaya kazuia mkutano na kututaka tuondoke bila kusema chochote”amesema Ndege.
 
Ameongeza kuwa ”Mimi ni Diwani wa CCM na tunatuhumiwa, siwezi kukaa kimya ni lazima nionyeshe ushirikiano wa kutatua hili tatizo na nikili kwamba nikweli ng’ombe zinaibwa Rorya na zinaletwa Bumera na wanagawana mchana kweupe waziwazi, ng’ombe 400 zimeibwa kuja hapa kwetu na tulishatoa taarifa majina ya wezi yako Polisi lakini hakuna uwajibikaji sasa Serikali haioni kuwa inakiweka chama cha CCM katika wakati mgumu? Na Mimi niliahidi kutatua tatizo hili na imefika wakati wananchi wameamua kujichukulia sheria mkononi kuua wezi jambo ambalo haliko kisheria” amesema.
 
Diwani wa Kata ya Kitembe, Thomas Patrick amesema kuwa aliomba kufanya mkutano huo kupitia Baraza la Madiwani na Madiwani wakakubaliana na kupanga tarehe ya mkutano uliopangwa kufanyika Kata ya Kitembe na kwamba kitendo cha kuzuia kimewakwaza.
 
  • Meya wa jiji la Dar atoa msaada wa kompyuta
 
“Labda alizuia kwakuwa mkutano ulikuwa unafanyika Kata ya Diwani wa Chadema lakini haukuwa wa kisiasa na taarifa OCD, RCO na RPC walikuwa nazo niliwaeleza kutakuwa na huo mkutano cha ajabu napigiwa simu na Afisa Tarafa kuwa Mkuu wa wilaya kasema mkutano usifanyike ungekuwa ni mkutano wa kisiasa Madiwani wa CCM wasingekuja nia yetu ilikuwa njema sisi Madiwani tumechaguliwa na wananchi yatupasa na sisi kushughulikia matatizo,”amesema Patrick.
 
Mwenyekiti wa Chama cha Mapunduzi CCM wilaya ya Rorya, Charles Ochele amesema mkutano huo haukuwa wa kisiasa bali ni mkutano wa ujirani Mwema uliowahusisha Madiwani kutoka Kata zenye mgogoro kufanya tatuzi ambao umeleta usumbufu kwa wananchi.
 
“Na ndiyo maana ukahusisha vyama vyote sisi wana Rorya ndiyo tunaumia mifugo inaibiwa na kupelekwa Tarime, wizi wa ng’ombe umekuwa ni kero Madiwani wa Tarime wamekuja kwa nia njema Rorya alafu Mkuu wa wilaya anazuia mkutano wananchi wanamfikiliaje ukizingatia yeye ni Mkurya na ng’ombe zinaibwa kutoka ujaruoni kwenda ukuryani hii inaleta picha mbaya itakayowafanya watu kuhisi tofauti.
 
Katibu wa Chama cha Democrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche amesema kuwa wao kama chama hawaoni kosa Diwani wa Chadema kushirikiana na Madiwani wa CCM katika shughuli za maendeleo zikiwemo za utatuzi wa kero mbalimbali kama wizi wa mifugo ambao umewakosesha amani wananchi wa Rorya kwakuwa Usalama wa Mali zao umepotea nakwamba zuio la Mkuu huyo limewashangaza.
 
Mbunge wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo (CCM) naye amekuwa akifanya mikutano katika vijiji mbalimbali vyenye changamoto za wizi wa mifugo ambapo baadhi ya wananchi walidiriki kuwataja hadharani wezi wa ng’ombe ambao aliagiza wakamatwe wakiwamo ndugu zake ambao hakuona shaka yoyote kuwakamata na kufikishwa Polisi ambapo baadhi yao kesi zao zinaendelea mahakamani na wengine waliachiwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha huku watuhumiwa wengine wakikimbia kuogopa kukamatwa.
 
Matukio ya wizi wa mifugo katika wilaya ya Rorya na Tarime yamekuwa yakitokea kila mara jambo ambalo limesababisha chuki na kuleta hofu juu ya usalama wa Maisha ya wananchi na mali zao, hivyo Wananchi wanaiomba Serikali kutatua suala la wizi wa mifugo ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.
 
Ikumbukwe kuwa miaka 10 iliyopita kabla ya Serikali kuanzisha Mkoa wa Polisi Tarime/ Rorya kwa kuongozwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya, Constantine Masawe wilaya hizo zilikabiliwa na mapigano ya kikabila na koo ambayo chanzo chake kilitokana na wizi wa mifugo na migogoro ya ardhi.
 
Kwa mujibu wa Takwimu za Polisi wakati wa uongozi wa Masawe zinaonyesha kuwa mapigano ya koo kwa mwaka 2008-2009 yalisababisha vifo kwa zaidi ya watu 52,wengine 91 kujeruhiwa na nyumba kadhaa kuchomwa moto huku ekari 49 za mazao ya chakula zikiharibiwa na kusababisha kutokea kwa njaa.
 
Vita hiyo ya koo jamii ya kabila la Wakurya Wilayani Tarime ilitokea mwaka 2008 mapigano kati ya Wasweta na Wahunyaga, Wanchari na Wakira, Wanchari na Wakira, Wanchari na Warenchoka na mwaka 2009 yalitokea mapigano ya kikabila kati ya kabila la Waluo waishio Wilayani Rorya na Wakurya koo ya Wamera waishio Kata Bumera Wilayani Tarime

LIVE: Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi barabara ya Mbinga- Mbambay mkoani Ruvuma
Mamlaka ya Maji Tarime yazindua bodi ya Maji