Siasa ni moja kati ya nyanja ambazo viapo vyake havipaswi kuaminika hata kidogo kwa kuwa hakuna urafiki au uadui wa kudumu, na mengi yanayotokea kwenye siasa huwezi kuyatabiri kwa macho ya kawaida au kwa kutumia historia ya wahusika.

Hebu fikiria, mwaka 2008 hadi mwaka 2014, kuna mtu aliwahi kuwaza kama Edward Lowassa atawahi kuwekwa kwenye bango la Chadema? Je, Kuna mtu aliwahi kufikiria japo kwa mbali sana kuwa mzee Kingunge Ngombale Mwiru ipo siku atapigia kampeni vyama vya upinzani na kuiacha CCM? Je, ulishawaza kufikiria kama ipo siku Dk. Slaa atakuwa timu moja na makada wa CCM na kuishambulia Chadema?

Kwa maswali hayo basi utakubaliana na mimi kuwa siasa ni zaidi ya kile tunachokiona, hivyo kesho yetu kwenye siasa na ibaki kuwa kesho hadi tutakapoiona ila ni muhimu sana kulifanyia kazi ipasavyo lililopo leo kwenye siasa.

Urafiki na uadui wa wanasiasa hutegemea na lengo na hali iliyopo kwa wakati husika. Endapo wanasiasa hao wana lengo moja, watakubaliana na kusifiana kwa namna zote. Lakini endapo wanatofautiana katika lengo lao, wanasiasa huvaana na hata kusababisha athari kubwa kwa wafuasi wao ambao huwaamini kwa asilimia zote.

Kwa kuzingatia utangulizi nilioutoa, ndi sababu leo hii tunaona majukwaa ya siasa ya CCM yanatumika kumsifia aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, ambaye alishambuliwa na makada na viongozi wote wa CCM wakati anagombea nafasi ya urais mwaka 2010 kwa tiketi ya Chadema.

Jana, mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli alimwagia sifa tele Dk. Wilbroad Slaa kuwa ni mtu safi na anayesimamia haki na anayepinga ufisadi kwa vitendo. Kauli ambazo hakika asingeweza kuzitoa mwaka 2010.

Bila shaka, uamuzi huo wa Dk. Magufuli umekuja baada ya Dk. Slaa kuonesha msimamo wake wa kumpinga mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa kwa madai kuwa ni fisadi na asiyefaa kuongoza taifa la Tanzania.

Dk. Slaa alitangaza kuachana na Chadema kwa madai kuwa hakuridhishwa na uamuzi wa chama chake kumpokea na kumpa nafasi ya kugombea urais. Nafasi ambayo alikuwa nayo Dk. Slaa tena kwa kuungwa mkono na vyama vingine vitatu vya siasa kama ilivyo sasa kwa Lowassa.

Baada ya kutangaza msimamo huo, Dk. Slaa aligueka kuwa malaika na rafiki wa CCM kwa kuwa tayari walianza kuongea lugha moja na kumnyooshea kidole adui yao mmoja, Edward Lowassa. Hapo msemo wa ‘Adui wa adui yako ni rafiki yako (An enemy of my enemy is my friend), ukatimia.

Zikiwa zimebaki siku 20 kabla watanzania kupiga kura, Dk. Magufuli alipanda jukwaani na kutumia dakika kadhaa kumsifia Dk. Slaa, huku kukiwa na taarifa kuwa mwanasiasa huyo mkongwe amepanga kupanda katika jukwaa la ACT-Wazalendo kwa nia ya kumvaa Lowassa.

Uamuzi wa Dk. Slaa ulikuwa habari njema kwa Dk. Magufuli na timu yake. Hivyo, hii ilionesha dhahiri kuwa wasomi hao wameungana rasmi dhidi ya adui yao mmoja, Edward Lowassa anaeonekana kuwa na nguvu kubwa na kusababisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa uchaguzi wa kihistoria wenye ushindani ambao haujawahi kutokea kwenye chaguzi zote Tanzania tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.

Ingawa hakuweka wazi, uamuzi wa Dk. Slaa kupanda jukwaani kumshambulia Lowassa una maanisha kumsaidia Dk. Magufuli kwenye vita hii kali ya kisiasa ya kuwashawishi watanzania.

Hata hivyo, uongoziwa ACT-Wazalendo, jana ulieleza kuwa umeshindwa kumpandisha Dk. Slaa jukwaani katika mikutano yao kwa sababu za kiusalama hivyo wakamshukuru tu kwa nia yake ya kutaka kuungana nao. Muungano ambao pia unatafsiriwa kuwa muungano wa kimkakati wa Dk. Slaa dhidi ya Lowassa.

Kwa mantiki hiyo, Dk. Magufuli na Dk. Slaa wameungana rasmi dhidi ya hasimu wao Edward Lowassa anaeonekana kuwa na nguvu kwa kuangalia mikutano ya kampeni anayoifanya. Kama nilivyoeleza awali, urafiki wao ni urafiki wa kisiasa usiotabirika wenye lengo moja la kimkakati la kuung’oa ‘mbuyu’.

Je, urafiki huu wa kisiasa zina msaada wowote katika harakati za Dk. Magufuli kuingia Ikulu kwa kuzingatia hali ya kisiasa nchini?

Ukaguzi Wa PPRA: NEC Miongoni Mwa Taasisi 9 Kupelekwa Takukuru Kwa Harufu Ya Rushwa
Mgombea Ubunge CCM Amsifia Lowassa