Na Josefly
Karibu tena kwenye ‘Throwback Thursday’ (TBT), Alhamisi ya kumbukizi ya yaliyojili na yakaacha alama kwenye kiwanda cha burudani ndani na nje ya +255.
Miaka 15 iliyopita, Juma Kassim Nature kutoka Temeke alikuwa moja kati ya wasanii watatu wenye majina makubwa zaidi kwenye mkondo mkuu wa Bongo Fleva. Albam yake ya kwanza, ‘Nini Chanzo’ pamoja na vibwagizo vikali kwenye nyimbo za wasanii wengine wakubwa zilikuwa chanzo.
Nature, ambaye alikuwa Mfalme wa Temeke wakati huo, aliitikisa Bongo baada ya kuanza uhusiano wa kimapenzi na Malkia wa tasnia ya maigizo wakati huo, ‘Sinta’.
Uhusiano huo ulikorezwa umaarufu kupitia masimulizi mengi yaliyokuwa yanaanikwa kwenye magazeti pendwa aka magazeti ya udaku. Kila uchwao, ilikuwa ni habari ya Juma Nature na Sinta ndizo zinazouza zaidi magazeti hayo. Kwa wale ambao tumezaliwa miaka ya 2000, Juma Nature na Sinta ndio ‘couple’ maarufu iliyowahi kutikisa zaidi kama ilivyowahi kuwa kwa Wema Sepetu na Kanumba au Wema Sepetu na Diamond. Kwa nje ilikuwa kama P.Diddy na J.Lo.
Hata hivyo, mapenzi hayo maarufu yalienda mrama, yakiwa na drama nyingi zilizozua gumzo kubwa kwenye magazeti, vipindi vya redio vya burudani pamoja na vijiwe. Enzi hizo hakukuwa na mitandao ya kijamii, hivyo masimulizi ya mdomo ndiyo yaliyotawala zaidi. Na kama unavyojua, masimulizi ya mdomo huongeza chumvi na kukoreza utamu au hata kuharibu mboga.
Moja kati ya mambo mazito yaliyokuwa yanatajwa kwenye harakati za vuguvugu hilo, ilikuwa tetesi za usaliti wa Sinta. Eti ikadaiwa Sinta alimsaliti Juma Nature kwa kuwa na uhusiano na wasanii kadhaa wakubwa wakati huo, mmoja ni marehemu na aliyekuwa na heshima kubwa kwenye muziki akitokea Mwanza.
Wakati huo, Sinta aliyekuwa akisoma Chuo cha Uandishi wa Habari cha DSJ jijini Dar es Salaam, baadaye alipata kazi ya kuwa mtangazaji wa Clouds FM jijini Mwanza, huko nako skendo za usaliti zikamfuata na magazeti yakachombeza kwelikweli eti anatembea na matajiri wa wauza samaki.
Hatimaye, kama waswahili wasemavyo, ‘ngoma ivumayo sana hupasuka’. Penzi la wawili hao ambalo linadaiwa kuwa liliunganishwa na muigizaji mwenzake Sinta, Swebe likavunjika na kishindo cha mvunjiko wake kilikuwa zaidi ya ule wa bawaba.
Ni zaidi ya ulivyowahi kusikia ‘Diamond na Wema wapigana chini’. Hii ya Juma Nature na Sinta, ilikuwa kali kwa sababu utamu wake ulikuwa wa masimulizi tu, ni kama kusikiliza mechi ya Simba na Yanga kwenye redio, unaweza kudhani na Barcelona na Real Madrid wanacheza. Si unajua tena maneno huumba pepo katikati ya dunia.
Baada ya kipindi kifupi, Juma Nature aliyethibitisha kuachana na Sinta, alitangaza kuwa ataachia albam yake ya mpya aliyoibatiza jina la ‘Ugali’. Akaahidi kuwa atasimulia yote kwenye albam hiyo. Kila mwenye pumzi na apendaye Bongo Fleva alipata ‘umateumate’, watu wakasubiri kwa hamu ugali wajue mbivu na mbichi.
Wanaume wakaendelea kushinda jikoni wakipika ‘Ugali’. Wapishi wakuu ni P-Funk Majani na Juma Nature, jiko lilikuwa Studio za Bongo Records.
Mara ikatangazwa rasmi kuwa ‘Ugali’ umeiva, na kwamba utapakuliwa kwa mara ya kwanza kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Ukumbi ambao hata wasanii wa kimataifa walikuwa wanasita kufanyia maonesho yao kutokana na kuogopa kupwaya.
Kama alivyoahidi, nyimbo zilizokuwa kwenye albam hiyo, tatu zilikuwa zinahusu sakata hilo. 1. Inaniuma Sana 2. Staki Demu 3. Sitaki Demu Remix. Nyimbo nyingine kwenye albam hiyo ni 4. Salio la Vesi 5. Aaah Wapi 6. Umoja wa Tanzania 7. Ugali.
Katika albam hiyo, ‘Inaniuma sana’ ambao uliokuwa mrefu, ulizungumzia kwa kina uhusiano wao tangu walipokutana na hata kusalitiana. Juma Nature aliimba kwa maumivu na uwasilishaji wake ulifanikiwa. Sanaa ikawateka watu wakamuamini yeye, hawakusikia upande wa Sinta.
“Siku ya kwanza kukutana naye, alikuja kwetu usiku/ alikuta nimechoka nimetoka kurekodi usiku. Walikuwa kama wanne hivi ndani ya gari aina ya Chaser/Wamejaa hangover utadhani jana yake walikesha. Akaja Mshikaji mmoja kutoka kwenye lilelile gari/akaja moja kwa moja hadi kwenye mlango wa ghetto, ‘Nature-Nature kuna mtu anakuhitaji hebu toka umuone….(huyu mshikaji ndiye anayedhaniwa kuwa alikuwa Swebe)….
Kwa maelezo ya Nature, msichana aliyetoka kwenye gari alikuwa na umbo ua uigizaji na alimuomba awe naye waende kula bata Billicanas Club (ukumbi wa Mheshimiwa Mbowe ambao ulishavunjwa, usiutafute hauko kwenye ramani tena). Na Nature alimkubalia kwa mujibu wa ngoma hiyo, so ni kama Sinta ndiye aliyepambania uhusiano huo.
Kwa hakika huu ulikuwa wimbo bora zaidi wa masimulizi wakati huo, nadhani hadi leo ndio wimbo unaoweza kukimbizana na ‘Zari la Mentali’ kwenye historia ya nyimbo za masimulizi ya mapenzi ya Bongo Fleva zilizoshika sana.
Juma Nature alimtaja jina Sinta kisanii, akieleza kuwa alimsaliti na mlevi mmoja ndiye aliyetoboa siri.
“Huko tulikokwenda noma kweli, Sinta na jamaa mmoja si walinyonyana, ulimi njenjeee… hadi kupata ajali wakati mumewe yu safari…”
Watu wakaunganisha matukio, Sinta aliwahi kupata ajali ya gari akiwa na mwanamziki huyo kutoka Mwanza wakitoka kufanya video ya wimbo.
Wimbo ukashika, watu wakaukariri… Nature akadai ‘Demu wangu amepimwa amekutwa ana ngoma’.
Siku ya uzinduzi, Dar es Salaam na vitongoji vyake ilihamia Diamond Jubilee, Nature akaandika historia ya kuujaza ukumbi ule hadi ukatema. Kila mmoja alitaka awe wa kwanza kuula ugali uliokuwa unapakuliwa mle ndani. Ukitaka kujua Nature alifanya balaa, ni Sean Paul peke yake wakati huo ndiye aliyekuja kuujaza pia ukumbi huo, ingawa bado ya Nature ilifurika na kucheua sana. Kuanzia hapo, ndipo alipopewa heshima ya kuitwa Sir. (Sir. Juma Nature). Kwa Uingereza, Malkia ndiye anayeweza kukubatiza wadhifa wa Sir. kutokana na kazi nzuri uliyoifanya kwenye eneo lako.
Nature uso kwa macho na Sinta Mwanza
Baada ya uzinduzi huo, Sir. Nature na timu ya Bongo Records wakafanya ziara kwenye majiji na miji mikubwa yote kuwalisha watu ‘Ugali’. Kila walipofika, walaji walikuwa na njaa ya maana na kumbi zilifurika.
Alipofika Mwanza, Nature na timu yake walikosa ukumbi wa kuwaweka watu wale ugali pamoja, ikabidi show ipigwe kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Ikumbukwe kuwa wakati huo Sinta alikuwa Mwanza akifanya kazi kama mtangazaji wa redio. Jiji likazizima, watu wakala samaki kwanza kisha wakaelekea CCM kirumba kula ‘Ugali’.
Basi unaambiwa kivutio kikuu, Sinta naye alikuwa miongoni mwa wahudhuriaji akiwa na timu yake.
Kabla ya show, Juma Nature alifanya mahojiano na Radio Free Africa, mtangazaji alimuuliza msichana aliyemuimba kwenye Inaniuma Sana ni nani.
“Mbona hata mtoto mdogo anaweza kujua, unasikia kabisa nimemtaja jina,” Nature alijibu. Sasa kumbuka kwenye ile anavyosema kuna mlevi mmoja aliropoka… hapo alimtaja Sinta.
Kwa mujibu wa magazeti pendwa wakati ule, Sinta na timu yake walishindwa kuvumilia wakimsikiliza Nature akianika yote kwenye mdundo wa P-Funk pale CCM Kirumba. Watu wakiwa wamefurika wakiimba naye mstari baada ya mstari. Ikaripotiwa kuwa ilitokea fujo iliyoanzishwa na ‘Timu Sinta’ ambayo hata hivyo ilidhibitiwa baadaye.
Unaambiwa ilikuwa show ya aina yake, uwanja ulifurika kama kuna mechi ya Simba na Yanga kumbe ni Sir. Nature aka Kiroboto. Umati ule naufananisha na show ya bure ya Awilo Longomba aliyowahi kuipiga Mwanza wakati ule akiwa juu ‘mawinguni’ na Mobimba ya Mama. Kwetu Mwanza bwana, usiulize umejuaje.
Mauzo ya ‘Ugali’ yakapaa, ingekuwa Marekani tungesema labda yalifika ‘Platinum’, ‘Gold’ au ‘Silver’. Kibongobongo mfumo wetu ulikuwa hauruhusu kujua nakala ngapi kwa uhalisia. Albam zilikuwa zinauzwa kwenye kanda na sio CD au santuli. Mhindi ndiye aliyekuwa anajua ukweli wa nakala alizogonga, wezi nao walijua kunakili na kuuza tena. Lakini mauzo yake kwa kipimo ya kiafrika yalikuwa balaa. Mimi huwa nayafananisha mauzo hayo na yale ya albam ya Saida Karoli ‘Chambua Kama Karanga’. Ila naye ukimuuliza ilikuwa nakala ngapi, hawezi kujua.
Baadaye, tukaambiwa Sinta alifanya utovu wa nidhamu kwenye kituo cha redio alichokuwa akifanyia kazi na akaachishwa kazi. Akarudi Dar es Salaam kuendelea na fani yake ya maigizo ambayo alifanikiwa sana pia kutokana na uwezo wake pamoja na jina alilokuwa nalo.
Hivi sasa Sinta ni mmoja kati ya waandishi wa habari wenye elimu ya juu, aliwahi kuweka wazi kuwa alichukua Shahada ya Uzamili (Master’s Degree) nchini Uganda. Mengine, mfuatilie kwenye website yake, maisha yanaendelea na mambo ni mengi muda kiduchu.
Ugali itabaki kuwa kati ya albam tano bora za muda wote za Bongo Fleva.
Kwangu mimi kwenye hizo tano bora za muda wote, nyingine ni ‘Machozi Jasho na Damu’ ya Profesa Jay, ‘AKA Mimi’ ya Ngwair… hizo nyingine mbili nikuachie wewe pia.
Huwezi kuitaja historia ya Bongo Fleva bila kumtaja Sir. Juma Nature ambaye sasa ana umri wa miaka 39.
Ni msanii aliyefanikiwa kuitambulisha vizuri Bongo Fleva ndani na nje ya Tanzania. Aliwahi kushinda Tuzo ya Video ya Channel O (CHOAMVA), ya Most Gifted East (Video Bora ya Muziki-Afrika Mashariki), na amewahi kutajwa kuwania Tuzo za MTV Europe, kwenye kipengele cha Best African Act (Msanii Bora wa Afrika).
Tukutane tena Alhamisi ijayo, turudishe nyuma. Narudia, kama hujui unakotoka, hujui unakokwenda.