Na Josefly:
Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt aliwahi kusema, “kwenye siasa, hakuna kinachotokea kama ajali. Ukiona kimetokea kama ajali ujue kilipangwa ila imekuwa ajali tu wewe kukiona wakati huo.”
Lakini pia mwandishi nguli na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Mmarekani aliyebarikiwa kuishi miaka 93 akayaona mengi, Doug Larson alisema, “badala ya kumpa mwanasiasa ufunguo wa jiji, inaweza kuwa bora zaidi ukibadili kufuli.” Na Winston Churchill, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, yeye akapingana na waliodai siasa ni mchezo mchafu, yeye anaamini, “Siasa sio mchezo bali ni biashara inayohitaji umakini.”
Hakuna jipya kwenye siasa, yote yanayotokea leo yameshasemwa na yamewahi kutokea, ni vile tu tumeamua kutoyafukua na kujisomea kwa sababu “tuna mambo mengi, muda mchache!”
Mwanasiasa ni kama njiwa, kiuhalisia, ni rahisi kumkamata njiwa wa jirani na kuanza kumfuga ukimpa chakula kizuri. Atakuzalishia, atakusikiliza na atakupa furaha uitakayo hata kwa miaka mitatu, lakini akili yake siku zote huwaza nyumbani kwao. Njiwa mgeni huwa na ramani ya kwao chini ya mbawa zake kama Michael Scofield alivyokuwa na ramani ya gereza mgogoni. Ukishindwa kumfanya ajisikie alipo ni nyumbani, ipo siku usiyoijua “atarudi nyumbani.”
Turudi kwenye kichwa ulichosoma hapo juu. Machi Mosi, mwaka huu ilikuwa siku ya aina yake. Siku iliyobadili tena historia ya vyama vya upinzani nchini. Ile asset (mali) ya Chadema waliyojitwalia mwaka 2015 kutoka CCM ilirejea ilikotoka. Ni Edward Ngoyaji Lowassa, chuma kisichoshika kutu kwenye siasa, kilichokataliwa na kuchafuliwa na Chadema kwa miaka saba mfululizo (2008-2015), lakini kikaokotwa tena na Chadema haohao, kikasafishwa, kikang’aa mithili ya dhahabu iliyopita kwenye moto mkali na kukitumiwa kwa heshima kupeperusha bendera ya chama kuwania Urais.
Ni Lowassa huyuhuyu, aliyewahi kupigwa mawe mazito na kutupiwa tope na pande zote mbili kwa nyakati tofauti. Lakini wengi tunachokumbuka zaidi ni kashfa nzito ya Richmond iliyomkumba mwaka 2008 na kumlazimu kujiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu. Lowassa aliyekuwa jemedari wa CCM, alichangiliwa bungeni na wabunge wa vyama vyote baada ya Ripoti ya Kamati maalum ya Bunge chini ya Uenyekiti wa Dkt. Harrison Mwakyembe kusomwa ndani ya jengo hilo la watunga sheria.
Kwa faida ya asiyejua kuhusu Sakata la Richmond au amesahau kidogo ngoja niwakumbushe:
Kwanza Tanzania ilikuwa na mpango wa kujenga bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, ushindani ulikuwa mkali sana kwenye zabuni hiyo, lakini katika kivuli cha mengi ilipewa Kampuni ya Marekani iliyoitwa ‘Richmond Development. Hata hivyo, kampuni hii ilishindwa kufanya kazi.
Mwaka 2006, Tanzania ikapata tatizo la umeme, katika kuchukua hatua za dharura kampuni ile ile ya Richmond Development ilipewa kazi ya kusambaza majenereta kuzalisha megawatts 100 za umeme kwa Sh. 172 bilioni za Tanzania. Majenereta hayakufika kwa muda, na yaliyopofika hayakufanya kazi. Lakini kwa mujibu wa Ripoti ya Dkt. Mwakyembe yenye kurasa 165, Serikali ilikubali kulipa $137,000 kila siku kama sehemu ya mkataba. Kamati ya Mwakyembe ikabaini kuwa kampuni ile ni ‘hewa’, haipo duniani! Kwa ufupi ilikuwa hivyo na jumba lote akaangushiwa Lowassa. Itabaki story kama alivyosema Rich Mavoko.
Chadema wakiongozwa na Dkt. Wilbroad Slaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho walimtaja Lowassa kwenye orodha ya mafisadi tena kati ya watatu wa juu, waliyoizindua jijini Dar es Salaam. CCM nao wakaanzisha harakati za ndani zilizoitwa ‘Vua Gamba’ ikiongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Komredi Abdulrahman Kinana na Nape Nnauye, lengo ni kuwataka mafisadi kujiondoa kwenye chama hicho, na inasadikika kuwa ilimlenga pia Lowassa aliyekuwa na nguvu hata baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu. Lowassa alipigwa huku na huku. Baadaye CCM wakavutana, wakaishia kukubaliana na uhalisia kuwa hakuna anayeng’oka, wakanyooshana ndani kwa ndani.
Vita ya Ufisadi ilikuwa sera muhimu iliyowapa Chadema umaarufu mkubwa wa kisiasa, wakaanzisha oparesheni ‘Sangara’, wakawataka wa CCM ‘Wavue gamba wavae gwanda’.
Lakini utetezi wa Lowassa ulionekana una mashiko kwa mtazamo fulani, kwamba katika uchunguzi wa kashfa yote, yeye hakuwahi kuhojiwa. Hivyo, kilichoripotiwa na Kamati ya Dkt. Mwanyembe kilikuwa na mapungufu ya kukosa upande muhimu wa mhusika. Ripoti hiyo iliacha pengo ambalo ndio utetezi muhimu wa siku zote wa Lowassa, alisema “nilionewa… sikupewa nafasi ya kusikilizwa (natural justice)… tatizo ni Uwaziri Mkuu.”
Swahiba wake wa damu, Dkt. Jakaya Kikwete ambaye alikuwa Rais wakati huo, alisema, “hiyo ni ajali ya kisiasa.” Lowassa akaona isiwe tabu, akaubwaga Uwaziri Mkuu kisha akasema, “mwenye ushahidi aende mahakamani la sivyo akae kimya milele”. Hakuna aliyethubutu kwenda mahakamani hadi leo, kwanini? Hata mimi sijui.
Ingawa alipakwa tope jingi, nyota yake haikuguswa. Mwaka 2015, tafiti nyingi za mtaani (zisizo rasmi) zilimtaja Lowassa kuwa ndiye anayeongoza kuwa na nafasi ya kuchaguliwa kuwa Rais kupitia CCM. Lakini waliibuka pia washindani wake wakuu, aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe na aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Marehemu Samuel Sitta. Hawa walitifuana kwelikweli. Kukawa na Timu Membe, Timu Lowassa na Timu Sitta. Hadi dakika ya mwisho majina yao yalipokatwa na ‘Wazee’ wa Kamati Kuu kukinusuru chama kisipasuke. Wazee walitumia busara, wakawaacha wote, mwisho Halmashauri Kuu ikamchagua Dkt. John Pombe Magufuli ambaye hakuwa hata na kundi la watu kumi.
“Isingekuwa busara za wazee, chama hiki huenda kingepasuka vipande,” alisema Jakaya Kikwete alipokuwa anazungumza na wazee wa chama hicho jijini Dodoma, siku kadhaa baada ya Dkt. Magufuli kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati yeye akijiandaa kumkabidhi Uenyekiti wa chama.
Lowassa hakuridhishwa na utaratibu uliotumika kulikata jina lake kwenye kinyang’anyiro hicho. Yeye na timu yake wakiongozwa na Marehemu Mzee Kingunge Ngombale Mwiru walionesha wazi kutoridhika na matokeo hayo. Hasira zikafika mbali, kukawa na sintofahamu kuhusu kundi kubwa lililokuwa linamuunga mkono, umati wa baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha kupinga pia wakasimama na kuimba “tuna imani na Lowassa.” Wimbo ulikorea, Mwenyekiti Dkt. Kikwete akasema, “haijawahi kutokea, lakini tunasonga mbele.”
Hasira za Lowassa kunyimwa nafasi zilitazamwa kama fursa kwa Chadema na CUF. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akabadili gia angani, yeye na baadhi ya watu wake wakamuita Lowassa‘chemba’ na kumshawishi kujiunga nao. Wakamuahidi kumpa nafasi aliyoikosa CCM. Mbowe alisema, “mtaji wa chama cha siasa ni watu, na Lowassa alileta watu.”
Picha ya kwanza ya Lowassa akiwa katikati ya wajumbe wa kamati kuu ya Chadema iliposambaa, wengi walipatwa na mshtuko, awali hata Mbowe mwenyewe aliikana kwa makusudi. Lakini baadaye mambo yalikuwa wazi, Lowassa rasmi ndani ya Chadema! Kweli wakati mwingine ni rahisi kujua kuwa hata mtoto anayefanana na wewe anaweza kuwa sio wako, kuliko kujua ni wakati gani mwanasiasa anasema ukweli.
Kweli idadi ya waliomfuata Lowassa ilikuwa kubwa, na hata waliobaki ndani ya CCM wengine walikuwa mamluki, walikuwa bado ni wafuasi watiifu wa Lowassa na waligeuka kuwa wasaliti kwa ajili yake, na walisaidia kuwapa ushindi wapinzani kwenye baadhi ya majimbo. Vyama vitano vya upinzani vikakubaliana kumnadi Lowassa.
Ujio wa Lowassa kwenye vyama vya upinzani uliwagharimu na kuwanufaisha. Waliwapoteza majembe Dkt. Wilbroad Slaa na Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti wa CUF), wakasema potelea mbali tumeleta tingatinga. Walivuna akina Frederick Sumaye, Hamisi Mgeja, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Mzee Matson Chiz, Makongoro Mahanga, Laurence Masha na wengine wengi, orodha ilikuwa ndefu.
Lowassa aliwahamishia Chadema jukumu la kumsafisha kwa yale waliyokuwa wanamsema. Chadema walibeba jukumu hilo na kufanikiwa kwelikweli kumsafisha huku baadhi ya makada waandamizi wa CCM wakimtupia kila aina ya tope. Ilikuwa ni kama timu hizi mbili zimebadilishana magoli na ‘jezi’. Chadema walijitahidi kuhakikisha wanapangua hoja wakisema wamejiridhisha kuwa Lowassa alionewa. CCM wakakwapua sera ya ufisadi, Chadema wakahamia kwenye sera ya Mabadiliko, nayo pia wakanyang’anywa kimtindo. CCM wakabadili M4C kuwa Magufuli For Change. Ilikuwa mtiti wa kisiasa kuwahi kutokea. Wengine waliziita sarakasi.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema ambaye pia ni Mbunge machachari wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alifanikiwa kuwashawishi wafuasi wa chama hicho kuwa Lowassa sio mhusika wa sakata la Richmond. CCM wao wakaendelea kumng’ang’ania, Dkt. Mwakyembe mwenye ripoti yake akashindilia misumari kwelikweli. Hata waliokuwa marafiki zake nao wakamgeuka, akina Joseph ‘Msukuma’ Kasheku na Hussein Bashe. Humphrey Polepole ambaye sasa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, alifanya kazi kubwa ya kuhakikisha anamsiliba Lowassa ipasavyo.
Yakatimia maneno ya muanzilishi wa taifa la China, Mao Zedong, “Siasa ni vita isiyo na umwagaji damu, wakati vita ni siasa yenye umwagaji damu.” CCM na Ukawa walipigana vita nzito ya hoja kuwahi kutokea nchini.
Ingawa Lowassa hakushinda uchaguzi, aliwaneemesha wapinzani. Aliwapa Ukawa jumla ya viti 116 bungeni, maana yake aliongeza kwa kasi pato la ruzuku na kutanua wigo wa vyama hivyo akipata kura milioni sita dhidi ya kura milioni nane za Dkt. John Magufuli (CCM) aliyeshinda urais, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Ukawa waliteka Halmashauri za Majiji, Dar es Salaam, Tanga na Mbeya kwa mara ya kwanza.
Kishindo cha nguvu ya Lowassa kwenye kampeni kilitikisa hata vyombo vya habari nchini. Kishindo hicho kilibadili hata aina ya uandishi wa magazeti, vichwa vya habari vilikuwa vya aina yake. Mfano, ‘Mafuriko ya Lowassa’, ‘Balaa la Lowassa’, ‘Kila Kona Lowassa’, na hata gazeti la Mwananchi liliwahi kuweka picha ya umati mkubwa wa wafuasi wa Lowassa na kuandika ‘Sema Wewe’, yaani msomaji mwenyewe ajiwekee kichwa cha habari kwani mwenye macho haaambiwi tazama. Ilikuwa balaa, CCM iliwabidi wajipange kwelikweli la sivyo ‘wangeisoma namba wenyewe’.
Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliwahi kukiri kuwa Lowassa aliwapa wakati mgumu kwenye uchaguzi mkuu. Kilichowaokoa zaidi ni kwamba walikuwa na mgombea aliyekuwa anauzika kirahisi kwa wapiga kura. Dkt. Magufuli hakuwa na madoa, hakuwa na makundi na kazi yake ilimuuza zaidi ya maelezo.
Hata baada ya uchaguzi, Lowassa aliahidi kuendelea kukaa Chadema akidai huko kunampa furaha na amani. Akasema wanaodhani atarudi CCM wanaota. Akaahidi kuendelea kujenga ngome ya upinzani. Aliwashangaa waliorejea CCM tena wakiacha ubunge na kuhamia upande wa pili kisha kupewa tena ubunge uleule. Alisimama hata alipoitwa kwa mara ya kwanza na kuhojiwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Julai 2017. Kwa Kiswanglish, “Chadema wakarelax.” Wakaamini Lowassa ametia nanga upinzani. Wakasahau waliishi na mtoto wa jirani aliyekuwa ameghafirishwa tu na uamuzi mmoja wa familia yake.
Machi Mosi, Chadema waliamshwa usingizini wasiamini wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii, “Lowassa arudi CCM.”Hakuna aliyetegemea na hata kwa waliotegemea hawakujua ingekuwa siku hiyo. Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Vincent Mashinji aliliambia gazeti la Mwananchi, “ilikuwa surprise, hakuna aliyejua, sisi tuliona kama wengine walivyoona.”
Kwa ukubwa wa Lowassa na mchango wake kwa chama hicho tawala, alikuwa kada pekee wa upinzani aliyerejea CCM na kupewa mapokezi ya namna ile. Ilikuwa n ka “shujaa amerudi.”
Viongozi wa juu wote wa CCM wakiongozwa na Rais John Magufuli walimpokea katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya chama zilizoko Lumumba jijini Dar es Salaam. Mapokezi yake hayakuwa na mashambulizi yoyote dhidi ya upinzani, ujumbe mmoja muhimu ulisisitizwa, “amerudi nyumbani.”Kweli alipokewa na timu yote ya walezi wa chama, kuanzia Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu wa Itikadi na Uenezi na wengine wote. Mapokezi yake yanaeleza. Kwa mujibu wa Lowassa, Rais Magufuli alitaka amsindikize pia Monduli lakini majukumu yalimbana. Utaona huyu alikuwa nani kwenye familia ya CCM.
Hata yule swahiba wake wa siku nyingi aliyestaafu siasa, Rostam Aziz alikuwepo kushuhudia. Naamini Rostam naye alimshawishi, “siku hizi kwetu pazuri, rudi.”
Sababu halisi za Lowassa kurudi CCM
Swali hili lilipata majibu mengi sana huko mitandaoni. Lakini Lowassa mwenyewe alisema, “nimerudi nyumbani kwa sababu nimerudi nyumbani.”Nadhani jibu hili ndilo jibu sahihi kati ya majibu yote.Linajibu maswali yotekama tutakavyolidadisi.
Kupata undani wa jibu hili kwanza rejea maelezo niliyokupitisha awali, kwanini Lowassa aliondoka nyumbani kwao mwaka 2015? Nikupe mfano, mtoto anapoondoka nyumbani kwao kwa hasira za kunyimwa nafasi ya kukalia kiti kizuri, akahisi ameonewa, kisha akashawishiwa na jirani kwenda kwake akiahidi kumpa kiti hichohicho lakini mwisho akaishia kujaribu tu lakini asikipate, unategemea nini siku za usoni? Tena endapo baba atamuomba mwanaye arejee tu nyumbani kwani bado kuna mengi mazuri?
Lowassa hakuhamia Chadema kwa sababu alivutiwa na sera zao, wala hakuiacha CCM kwa sababu hakupenda sera zao. Aliondoka kwa ‘hasira’ za kuamini alionewa na hakutendewa haki na Kamati Kuu mwaka 2015. Kwa bahati mbaya, kilichomshawishi kuingia Chadema hakukipata, lakini bado hasira za ‘uonevu’ ule zilimjaa hivyo aliona bora abaki ‘ugenini’.
Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Magufuli aliliona hili, kama kiongozi akachukua jukumu la kumshawishi na kumrudisha mwana CCM nyumbani. Akamuita Ikulu Januari 9 mwaka jana, na kwa mujibu wa Lowassa alimshawishi kurejea CCM lakini kwanza alimkatalia. “Nilimwambia Mheshimiwa Rais uamuzi wangu wa kuhamia Chadema haukuwa wa kubahatisha.”
Rais Magufuli alionekana akimsindikiza mgeni wake nje ya mlango wa Ikulu na kumuaga vizuri. Alimuelezea kama ni kati ya wazee wa nchi waliofanya kazi kubwa.
Lakini miezi kumi baadaye, ni kama Lowassa alishusha pumzi ya hasira/kughafirishwa na ‘familia yake’, akalisiliza vizuri neno la wito wa kurejea nyumbani na hatimaye akakubali ombi la Rais Magufuli.
“Namshukuru Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo, na kazi kubwa aliyoifanya ya kunishawishi nirudi CCM. Amefanya kazi kubwa sana, ninamheshimu na namshukuru,” amesema Lowassa alipofika Monduli, jimbo aliloliongoza kwa miaka 20 kama mbunge wa CCM anayekubalika sana.
Kama Lowassa alivyosema katika hotuba yake Monduli, kuwa Rais Magufuli ni kiongozi wa maono (visionary Leader), kama Mwenyekiti wa CCM, amefanikiwa kumshawishi Lowassa na kumrudisha nyumbani akiona mbali. Ni kama ilivyofanya wakati ule Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe aliona mbali, akabadili gia angani akaamua kumnasa Lowassa hata kama ilibidi wengine waondoke ili mradi tu alijua angekuja na watu ambao kwa mujibu wake ndio mtaji wa chama cha siasa. Na kweli Mbowe alipata faida kubwa.
Cha kushangaza, kuna wanaomkosoa Lowassa eti ameondoka wakati Mbowe yuko rumande, wanasahau kuwa Mbowe alimuondoa CCM wakati CCM iko vitani, ulikuwa wakati muhimu sana kwa CCM kuungana, Lowassa aliwaachia hali ngumu. Waswahili husema, “mwiba unapoingilia ndipo unapotokea.” Yule mwana amerejea nyumbani kwao, jirani hapaswi kusikitika eti kwakuwa alimzoea sana na eti ameondoka katika kipindi kigumu kwake!
Kingine cha msingi na faida kubwa kwa Lowassa, ni kwamba sasa kisiasa ni msafi, tena “msafi kama pesa mpya”. Ingawa sina uhakika na usafi huo kwani yeye bado ni binadamu mwenye yake mengi. Nachoamini ni kwamba alisafishwa vizuri na Chadema pamoja na vyama vingine vinne vya upinzani, halafu amesafishwa tena na CCM wenyewe. Sasa hakuna wa kumrushia tope la zamani labda zibaki lawama tu, pande zote ni kama wamejiridhisha na wameona anawafaa.
Alipopokewa Monduli juzi kwa kishindo, alimgeukia Polepole na kumkumbusha kuwa alimsema sana lakini sasa wako pamoja wanajenga chama.
Usiulize itakuwaje.. usiwaze sijui sasa Polepole, Dkt. Mwakyembe, Nape, Msukuma na wengine wataishije na Lowassa ndani ya CCM hii kwa kuzingatia walivyomsema sana! Jibu ni rahisi, wahenga walisema, “ndugu wakigombana kashike jembe ukalime.” Na pia, kama aliweza kuishi kwa amani’ugenini’ walikokuwa wamemsema sana awali, itakuwaje nyumbani kwao?
Lakini pia, kama alivyowahi kusema Komredi Abdulrahman Kinana, “Lowassa ni muungwana na amekomaa kisiasa.” Katika hotuba yake ya mapokezi ya Monduli, hakuwarushia neno lolote baya Chadema. Aliwashukuru sana kwa kumpa nafasi. Aliomba asiwekewe maneno yoyote mdomoni, lake ni shukurani kwa viongozi na wanachama wa Chadema.
“La tatu, na mnisikilize vizuri, kwa Chadema nawaambia asanteni sana. Viongozi wa Chadema na wanachama wa Chadema, asanteni nawashukuruni sana. Sina zaidi, asanteni na nawashukuruni sana, msiniwekee maneno mdomoni,” alisema.
Naamini hakuna mwanasiasa mwingine yeyote aliyehama Chadema kwenda CCM au CCM kwenda Chadema bila kuwarushia makombora huko alikotoka, kwa sasa ni Lowassa tu aliyefanya hivi wakati huu.
Na nyie ndugu zetu wanasiasa, jitahidini kuwa na akiba ya maneno, mambo hubadilika, kuna kesho!
Kweli, dakika moja ya siasa ni sawa na miaka kumi ya maisha ya kawaida. Mengi yanaweza kutokea. Kwa sasa tuisikilize sauti ya Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Magufuli, “sasa ni wakati wa kuchapa kazi tu ili Taifa letu lizidi kusonga mbele.”
Siasa tusubiri Chaguzi za Serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.