Na Ghati:
Wingu zito la majonzi lilitanda juu ya anga la Afrika na Dunia kwa ujumla jana majira ya mchana, baada ya kutangazwa kuwa Sauti ya Afrika, Jiwe la Afrika na Gitaa la Haki, Oliver “Tuku” Mtukudzi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66.
Ulikuwa wakati mgumu kwa Zimbabwe ambayo siku zote iliikumbuka sauti ya Oliver Mtukudzi kama alama iliyochagiza kupatikana kwa uhuru wa nchi hiyo kutoka kwenye mikono ya makaburu. Sauti iliyowatetea, iliyowatoa machozi lakini pia iliyowafanya wacheze na kuruka kama ndama. Kwa ujumla alikuwa alama ya muziki wa Zimbabwe iliyokubalika duniani.
Alizaliwa September 22 mwaka 1952 katika mji mdogo wa Highfield, jijini Harare nchini Zimbabwe, wakati huo inaitwa Rhodesia. Akiwa miongoni mwa watoto sita wa mzee Mtukudzi, aliishi na kukulia katika mji huo uliokuwa na makazi duni. Alikuwa mtoto mwenye kipaji cha aina yake, aliyebarikiwa na Mungu kuitumia sauti yake kwa ajili ya wanyonge.
Akiwa na umri wa miaka 25, Oliver alijiingiza rasmi katika muziki wa kutumbuiza jukwaani. Mwaka 1977, alijiunga na bendi ya Wagon Wheels iliyokuwa na wanamuziki wenye vipaji vikali kama Thomas Mapfumo ambaye baadaye alipewa jina la ‘Simba wa Zimbabwe’ na mwingine ni James Chimombe aliyefariki dunia mwaka 1990.
Oliver ni jasiri ambaye hakuacha nyuma asili yake, alitumia lugha ya kabila la kwao ya ‘Shona’ inayozungumzwa zaidi nchini Zimbabwe ikimilikiwa na Washona pamoja na ‘Ki-Ndebele’
Hata hivyo, kwa lengo la kupaza sauti yake zaidi duniani, hasa akikemea ukandamizaji wa haki, alitumia lugha ya Kiingereza katika baadhi ya nyimbo zake.
Lakini alipotumia lugha ya Kiingereza, alihakikisha muziki wake una vionjo vya asili ya Afrika ikichanganywa na gitaa. Muziki huo ulimpa umaarufu zaidi na kumtofautisha na wengi hasa wageni na hiyo ndiyo sababu ya muziki wake kuitwa ‘Tuku Music’.
Nguli huyu alifahamu kuwa moja kati ya siri kubwa ya kufanikiwa duniani kimuziki, ni kuhakikisha muziki wako unakuwa na asili yako ili ujitofautishe na wengine na kukupa utambulisho wa pekee. Hii ndio sababu alipokutana na Lady Jay Dee wa Tanzania kwa mara ya kwanza katika tuzo za KORA nchini Afrika Kusini, Jide alipohakikisha haipotezi nafasi ya kuzungumza na nguli huyo akitaka kujua siri ya mafanikio, hili lilikuwa nguzo ya yote.
“Ni mtu ambaye nilikuwa namuona ni mwanamuziki mkubwa na anafanya muziki mzuri. Kwahiyo nikamkimbilia nikamfuata na baada ya hapo maisha yangu yalibadilika, kwa sababu ushauri alionipa kuhusiana na mambo ya kufanya ‘Live Music’ na kuhusisha vionjo vya Kiafrika kwenye muziki, amehusika kwa kiasi kikubwa kubadilisha muziki wangu,” Lady Jay Dee ambaye alipata bahati ya kufanya naye wimbo mmoja uitwao ‘Mimi ni Mimi’ amesimulia.
Kwakuwa muziki una lugha moja, Oliver alianza kuzunguka akiimba dunia akipewa mialiko kwenye matamasha makubwa ikiwa ni pamoja na nchi za nje ya Afrika kama Marekani, Uingereza na Canada, na alipewa heshima kubwa.
Kutokana na uwezo wake wa kutunga mashairi yanayoendana na hali halisi ya maisha, akilenga hasa kuwakomboa watu wa chini, hakukaukiwa mada nzuri kwenye nyimbo zake na kutengeneza albam nyingi pendwa.
“Huko nitokako mimi, hautakiwi kuimba wimbo wowote kama hauna jambo la kusema, kwahiyo kila wimbo wangu una jambo la kumzungumzia mtu ambaye yuko huko mitaani. Ni lazima aweze kuutumia katika maisha yake,” moja kati ya kauli za Oliver ‘Tuku’ Mtukuzi zilizo akikaririwa na CNN.
Aliachia albam yake ya kwanza mwaka 1978 na aliipa jina la ‘Ndipeiwo Zano’. Albam hiyo ilitoa matumaini na kusaidia kusukuma gurudumu la kudai uhuru kutoka kwa wakoloni huku ikiokoa maisha ya Wazimbabwe wengi waliokuwa wamekatishwa tamaa na unyonyaji, ukandamizaji na maisha ya mateso ya kikoloni. Mwaka 1979, ikiwa ni mwaka mmoja tu kabla ya uhuru wa nchi hiyo, alikandamiza tena kwa albam aliyoiita ‘Muroi Ndiani?’.
Katika kipindi chote cha maisha yake, alitoa jumla ya albam pendwa 59; albam ya mwisho ikiwa ni Han’a (Concern) aliyoiachia rasmi mwaka jana.
‘Nyoka huzaa nyoka’, Oliver alifanikiwa kupata watoto watano, na wawili kati yao walikuwa wanamuziki kama baba yao. Mwanaye Sam Mtukudzi alifanikiwa kuwa mwanamuziki maarufu nchini Zimbabwe, lakini mwaka 2010 alifariki kwa ajali ya gari.
Kama nilivyoeleza, nyimbo za Oliver Mtukudzi zilizingatia hisia halisi za maisha. Hivyo, mwaka 2012 aliachia albam aliyoiita ‘Sarawoga’ (kuachwa mpweke), ikiwa ni maalum kwa ajili ya mwanaye aliyefariki.
Mbali na muziki, Mtukuzi ambaye aliinuka kuwa mfanyabiara, alisaidia katika kufanya filamu kubwa zenye ujumbe wa aina yake kwa lengo la kutetea na kuokoa maisha ya wanyonge.
Filamu ya Neria ya mwaka 1993, inakumbukwa zaidi kama moja kati ya filamu alizozing’arisha. Alikuwa miongoni mwa wahusika wakuu na aliimba wimbo wa filamu hiyo ulioiuza zaidi filamu hiyo iliyopinga unyanyasaji wa mwanamke katika mirathi.
Filamu nyingine alizoshiriki ni pamoja na Jit ya mwaka 1990, Shanda ya mwaka 2002, Sarawoga ya mwaka 2009 pamoja na Nzou NeMhuru Mudanga ya mwaka 2012.
Kutokana na kazi yake nzuri, kama mwanamuziki na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu, alitunukiwa tuzo kubwa na za heshima zaidi ya 25. Tuzo hizo zilitolewa na taasisi mbalimbali za burudani, taasisi za kimataifa za masuala ya jamii pamoja na vyuo vikuu mbalimbali.
Mwaka 2011, alichaguliwa kuwa Balozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) wa Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Alifariki Januari 23 akiwa na umri wa miaka 66, katika Hospitali ya The Avenues jijini Harare, alipokuwa akipatiwa matibabu kutokana na ugonjwa wa kisukari aliokuwa nao kwa muda mrefu. Umauti umemkuta ikiwa ni mwaka mmoja kamili tangu rafiki yake kipenzi, Hugh Masekela atangulie mbele za haki
Huyo ndiye Mtukudzi, ‘Jiwe la Afrika’, ‘Sauti ya Afrika’, maarufu zaidi kama ‘Tuku’. Ingawa hatuko naye tena, muziki wake utaishi hadi mwisho wa dunia.
Pumzika kwa amani ‘Tuku’, gitaa lako litabaki na upweke lakini muziki wako utaendelea kuipa dunia faraja.