Na: Josefly Muhozi

Oktoba 11, 2019, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed alitajwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kumaliza vita na taharuki ya kijeshi kati ya nchi yake na Eretria. Atakabidhiwa tuzo hiyo pamoja na kitita cha $900,000 (Sawa na Sh 20.7 bilioni za Tanzania).

Unaweza kujiuliza, fedha hizo zimetoka wapi? Ni tone la utajiri aliouacha muasisi wa tuzo hizo, Alfred Bernhard Nobel, raia wa Sweden aliyeishi kati ya Oktoba 1833 na Desemba 1896. Nobel aliyeishi miaka 63, alitumia miaka yake yote kujifunza na kutengeneza silaha nzito za kuua watu wengi na kwa haraka lakini mwaka mmoja wa mwisho alibadilika baada ya ‘kuuawa na vyombo vya habari’ na kusikia dhahiri shahiri dunia inavyomsema baada ya ‘kufa’. Fuatilia makala hii utaelewa zaidi.

Alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto nane wa mwanasayansi mbobezi na mvumbuzi, Immanuel Nobel, ni kati ya watoto wanne pekee katika familia yao walioweza kuvuka umri wa utoto, ndugu zake wanne wote walipoteza maisha wakiwa watoto.

Baba yake alikiona kipaji chache cha udadisi, kwakuwa alipenda kufuatilia kazi alizozifanya. Hivyo, 1842 walimpeleka kwa mwalimu binafsi aliyemfundisha somo la kemia pamoja na lugha kama Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kirusi. Pia, alijiandikisha na kupata elimu katika shule pekee aliyosoma akiwa mdogo kati ya mwaka 1841 hadi 1842 iitwayo Jacobs Apologetics iliyopo jijini Stockholm.

Alianza kuvutiwa na somo la kemia hasa baada ya kusoma na mkemia Nikola Zinin. Yeye alipendelea zaidi kutumia uweledi wake kuunda silaha mbalimbali na vilipuzi; na kwa msaada wa Zinin alifanikiwa kuanza kutengeneza baruti. Alipohamia jijini Paris nchini Ufaransa, alikutana na Ascanio Sobrero aliyekuwa amevumbua kilipuzi cha kimiminika cha nitroglycerin.

Ingawa Sobrero alipinga matumizi ya kilipuzi hicho alichokivumbua mwenyewe, Nobel yeye alivutiwa zaidi, alitaka kukifahamu zaidi akieleza kuwa ni biashara nzuri. Jamaa alikuwa na jicho la kijasiriamali lenye ubinafsi.

Kwa bahati, baba yake alianzisha kiwanda cha kutengeneza silaha za kivita ikiwa ni pamoja na vilipuzi. Walifanya biashara nzuri wakati wa vita kati ya Dola ya Kirumi na Dola ya Ottoman, mwaka 1853 hadi 1856 iliyomalizika baada ya Dola ya Kirumi kushindwa. Baada ya vita hiyo, kiwanda cha familia ya Nobel kiliyumba sana kibiashara, wakatangaza mufilisi.

Hata hivyo, mwaka 1859, baba yake aliamua kujiondoa kwenye kiwanda hicho na kumuachia kaka yake Alfred aitwaye Ludvig Nobel ambaye alikiendeleza na kufanikiwa. Wakati huo, Alfred Nobel aliendelea kujikita katika utafiti wa kutengeneza kilipuzi cha nitroglycerin hadi alifanikiwa.

Kwa bahati mbaya, kilipuzi cha kwanza cha nitroglycerin kililipuka kama ajali ndani ya kiwanda chao na kusababisha vifo vya watu watano akiwemo mdogo wake wa tumbo moja, Emil. Kilipuzi hicho pia kilijeruhi wafanyakazi wengi.

Tukio hilo la kusikitisha kwake lilikuwa kama majibu ya mafanikio ya kilipuzi alichokihangaikia. Alitembea sehemu nyingi duniani akitafuta namna ya kukiboresha. Yeye alikuwa mfuasi wa msemo wa Kiswahili, ‘atafutaye hachoki, akichoka ameshapata’. Hivyo, mwaka 1865 alifanikiwa kugundua kilipuzi kinachojulikana kama ‘blasting cap’. Na mwisho alifanikiwa kuvumbua kilipuzi kizito zaidi kinachofahamika kama dynamite na baadaye ‘ballistite’ ikitoholewa kutoka kwenye ballistae’. Milipuko hiyo ilitumika kuua watu vitani na yeye aliingiza fedha nyingi sana. Hiyo ni kama kusema alikuwa akipokea fedha za damu.

Hata hivyo, maisha ya Alfred Nobel yalikuwa na misukosuko mingi hasa kwenye uhusiano wa mapenzi, na ni moja kati ya vitu vilivyomtesa sana. Hakufanikiwa kuoa ingawa kumbukumbu zinaonesha kuwa aliwahi kuwa na wapenzi watatu waliofahamika kwa watu wengi. Mpenzi wake wa kwanza aliyefahamika alikuwa anaitwa Alexandra, raia wa Urusi.

Lakini mwanamke aliyedaiwa kumpa msongo mkubwa wa mawazo na kumfanya kuishi maisha ya shida licha ya utajiri alionao ni mrembo na mwandishi Bertha Von Suttner. Inaelezwa kuwa alimpa ukichaa wa mapenzi Nobel hasa alipomkatalia ombi lake la kutaka wafunge ndoa.

Akiwa mzee sana na mwenye msongo mzito wa mawazo, Nobel alikutana na mtihani uliobadili kabisa maisha yake. Waingereza wanasema ‘a turning point of his life’. Uzushi uliovuma ulimpa somo la aina yake, naye kwakuwa ana historia ya kuwa mwanafunzi mzuri, uzushi ule ulimfunza somo zito, akahitimu ndani ya siku chache na kubadili maisha yake yote.

Ilikuwa hivi, mwaka 1888, kifo cha kaka yake, Ludvig Nobel kilisababisha magazeti mengi kuandika kuwa aliyekufa ni yeye, yaani Alfred Nobel.

Tofauti na uvumbuzi mkubwa alioufanya ambao unatumika hadi leo, magazeti mengi yalimuandika vibaya. Gazeti moja maarufu la Ufaransa liliandika ‘Le marchand de la mort est mort’, kwa kiingereza ‘The merchant of death is dead’(Mfanyabiashara wa kifo amefariki).

Kwenye taarifa hiyo, ilimuelezea Alfred Nobel kuwa alikuwa mfanyabiashara aliyehangaika kutafuta silaha ambazo zitaua watu wengi kwa haraka zaidi ya ilivyokuwa awali. Kwakuwa alikuwa hajafa, Alfred aliisoma habari hiyo mstari kwa mstari na akabaini kuwa atakapokuwa amekufa hatakumbukwa kwa mema bali atakumbukwa kwa mabaya, kama ‘wakala wa kifo!’ Akabadili gia angani, akatubu na kuamua kuwekeza mali zake zote kuwatuza wanaofanya kazi nzuri ya kuboresha maisha ya watu kwa kujitolea, ubinadamu kwanza.

Hatua hiyo ilimfanya aanzishe tuzo za Nobel mwaka 1895. Na mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1986 alifariki dunia. Inaelezwa kuwa yule mrembo ambaye alikataa ombi lake la kumuoa, Bertha Von Suttner ndiye aliyemshawishi kuweka kipengele cha amani kwenye tuzo hizo. Huenda alimkatalia kwa sababu aliona atakuwa na mume ambaye anahangaika kila siku kutafuta pesa kwa kutengeneza vifaa vinavyoua watu kwa kasi zaidi.

Nobel aliacha wosia ambao ulipelekea kuanzishwa kwa ‘Foundation’ yake Juni 29, 1900 ambayo moja kati ya majukumu yake ni kusimamia  mali na fedha alizoziacha kwa ajili ya kutoa tuzo zinazofahamika kwa Kiingereza ‘Nobel Prizes’. Alitoa asilimia 94 ya mali zake kwa ajili ya kuwatuza watu wanaofanya vizuri kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu kwenye maeneo ya kemia, fizikia, saikolojia au tiba/dawa, fasihi na amani. Wahusika ni wale wanaojitoa kwa ajili ya ubinadamu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tuzo za Nobel anateuliwa na Mfalme wa Sweden na wajumbe wengine wanne wa bodi watachaguliwa na mamlaka nyingine inayoaminika.

Tangu kuanzishwa kwake, waafrika 24 wameshinda tuzo hiyo ambayo inatajwa kuwa tuzo kubwa zaidi na yenye heshima zaidi duniani. Na mwafrika wa 24 ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed aliyetangazwa mwishoni mwa wiki hii.

Kishindo cha JPM, Ahamia rasmi Dodoma
Jafo ataja Mikoa iliyozorota uandikishaji, wakuu wa mikoa kitanzini