Bondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo ametembelewa na nyota ya bondia Mfilipino, bingwa wa dunia wa masumbwi uzito wa Welterweight ambaye pia ni Seneta nchini kwake, Manny Pacquiao baada ya mwanzo wa historia yao kwenye ulimwengu wa masumbwi kufanana.

Mbali na historia ya Mwakinyo ulingoni kufanana na ya Pacquiao, historia ya nje ya ulingo na maisha ya mtaani pia vina mfanano wa hali ya juu, ikiwa wawili hao walitumia dakika chache walizopewa kama ‘waziba pengo’ kwenye pambano muhimu kuishangaza dunia.

Usiku wa Jumamosi, Septemba 8 mwaka huu ulikuwa usiku ambao dunia ilishuhudia Tanzania iking’ara kwenye kilele cha mchezo wa masumbwi duniani, baada ya bondia Mtanzania Mwakinyo kumshushia kipigo kisichotarajiwa bondia anayeshika nafasi ya nane kwa ubora duniani, Sam Eggington, katika pambano lilifanyika Birmingham nchini Uingereza.

Hassan Mwakinyo akimshushia kipigo Sam Eggington

Mwakinyo ambaye hakuwa anafahamika kwenye ulimwengu wa Masumbwi, hata hapa nyumbani pia jina lake lilikuwa chini, alipewa taarifa za kupambana na mbabe Eggington ndani ya wiki mbili, baada ya bondia aliyekuwa amepangwa kupata udhuru. Wawili hao walipambana kwenye pambano la utangulizi la pambano ambalo lilikuwa kubwa zaidi duniani usiku huo kati ya bondia Amir Khan na Samwel Vargas.

Mwakinyo alimnyanyasa ulingoni Eggington kwa masumbwi mfululizo na kulimaliza pambano ndani ya dakika chache (raundi ya pili). Kabla ya pambano, Mwakinyo alipewa alama 1 kati ya 20 (1/20) ya uwezekano wa kushinda. Ikumbukwe kuwa mpinzani wake aliwahi kuwa bingwa wa masumbwi uzito wa Welterweight wa Ulaya, bingwa wa masumbwi wa Jumuiya ya Madola na mengine.

“With only 1 week notice he destroyed Eggington wow,” ujumbe huu wa shabiki aliyeandika kwenye akaunti ya YouTube ya SkySports inafanana na alichokisema mshereheshaji wapambano la kwanza la Pacquiao Marekani.

Historia hii ya Mwakinyo, inafanana kabisa na ile ya Manny Pacquiao, ambapo Juni 23 ya mwaka 2001, Pacquiao alipata nafasi ya kupanda ulingoni kwa mara ya kwanza nchini Marekani, katika ukumbi maarufu wa ndondi wa MGM Grand wa Las Vegas. Hakuna aliyekuwa anamjua Manny Pacquiao kwenye ulimwengu wa masumbwi ya orodha A wakati huo.

Manny Pacquiao akimuadhibu Lehlo Ledwaba mwaka 2001

Pacquiao, kama ilivyo kwa Mwakinyo alipanda ulingoni siku hiyo kuziba pengo la bondia aliyekuwa amepangwa kupambana na bingwa wa dunia wa masumbwi wa IBF, uzito wa super bantamweight, Lehlo Ledwaba. Ledwaba alikuwa na historia nzuri ya kushinda mapambano 31, kushindwa 1 na kutoa sare 1. Huku Pacquiao akiwa na historia nzuri nyumbani kwao Ufilipino, Marekani na dunia havikuwa vikimpa nafasi ya kupona mikononi mwa Ledwaba.

Lakini, ndani ya raundi chache, Pacquiao alimnyanyasa Ledwaba na kumshinda kwa TKO, na tangu hapo sio tu jina lake bali hata jina la nchi yake ya Ufilipino ni maarufu katika dunia ya masumbwi. Baada ya pambano hilo, Pacquiao alikuwa ‘keki’ inayofukuziwa na makampuni ya ngumi duniani. Mikataba minono ilimiminika.

Hali hiyo pia imemtokea Mwakinyo, ambaye baada ya kumtwanga Eggington, mikataba minono imefululiza kwake na hata kampuni ya Bingwa wa Dunia wa Masumbwi ambaye alistaafu bila kupigwa katika mapambano 50, Floyd Mayweather kupitia ‘The Money Team’ imemtaka.

“Kilichonishtua zaidi ni kuitwa na kampuni ya TMT ambayo inamilikiwa na bondia Floyd Mayweather, nimeshangaa sana. Dakika 15 tu zimeniwezesha kuwashangaza wadau wa ngumi za kulipwa duniani,” amesema Mwakinyo.

Mwaka huu, akiwa kama Seneta, Pacquiao alimpiga bondia Lucas Mattysse, pambapo lililohudhuriwa na Rais Rodrigo Duterte. Leo Pacquiao anaitwa ‘Ngumi ya Taifa’ (Fist of the Nation). Hivi sasa anashika nafasi ya 4 kwa ubora duniani akiwa anatajia kustaafu.

Mfanano wa nyota; maisha ya kujifua/umasikini:

Pacquiao anafahamika zaidi kuwa ametokea kwenye maisha ya hali duni, akikulia katika mitaa ya jiji la General Santos, South Cotabato.

Katika mitaa hiyo alikuwa na chumba ambacho hata hakukuwa na hewa nzuri ndani. Akiwa na rafiki zake walifunga gunia la kutengeneza na humo ndani walianza kujifua kwa masumbwi. Katika mwanzo huo, kwa umasikini wa wazazi wake ambao hata hivyo walikuwa wametengana hakuweza hata kununua vifaa vya mazoezi. Lakini uwezo wake na jitihada vilimuinua, akakutana na wadhamini waliouona uwezo wake na kumpeleka Marekani kujaribu bahati yake miaka michache baadaye.

Haikuwa rahisi kwa Pacquiao kufanikiwa kufanya mazoezi kwenye ‘gym’ ya Wild Card na kuanza kufuliwa na Freddie Roach, mkufunzi aliyedumu naye kwa miaka zaidi ya 15 akizoa mataji.

Kama ilivyo kwa Pacquiao, Mwakinyo ni mzaliwa wa jiji la Tanga eneo la Makorora ambaye ametokea katika maisha ya kimasikini. Hali duni imemfanya kushindwa hata kununua vifaa vya mazoezi, licha ya kupenda mchezo huu.

“Natoka kwenye familia masikini ambayo hata uwezo wa kununua gunia la mazoezi haina, natumia tairi la gari kufanyia mazoezi, tena siyo kwenye ‘gym’ katika uchochoro wa mtaani,” Mwakinyo aliiambia Mwananchi kwenye mahojiano maalum.

Leo, Pacquiao ana historia nzito, akiwa ni bondia wa kwanza kushinda mataji muhimu manne ya dunia kwenye uzani nane tofauti kama vile flyweight, featherweight, lightweight  na welterweight. Amepewa heshima ya kuwa ‘Mpiganaji wa Muongo’ (Fighter of the Decade).

Anatarajiwa kuwania nafasi ya urais wa Ufilipino mwaka 2022, na tayari amepewa baraka hizo na Rais Duterte.

Ndondi za miaka zaidi ya 25 zimemfanya auage umasikini, na mwaka 2015 alitajwa kushika nafasi ya pili baada ya pambano lake na Mayweather kama mwanamichezo aliyeingiza fedha nyingi zaidi ($160 milioni), akifuatiwa na Cristiano Ronaldo aliyekuwa na $79.6 milioni.

Tumuunge mkono Mwakinyo, anarejea nyumbani kuipitia mikataba yote aliyoahidiwa, kwa kushirikiana na Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa (TPBRC) watafanya maamuzi sahihi, na Tanzania tutazidi kung’ara duniani.

Nimefurahishwa na kauli ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kwa namna wanavyopanga mkakati wa kumsaidia.

“Atakapofika nchini tutakaa naye kujua tunamsaidia vipi katika pambano lake la Ujerumani, lazima tumsaidie, sasa hivi atakuwa akiangaliwa na mabondia wakubwa zaidi lakini ili afike mbali ni lazima twende kimkakati,” alisema Dkt. Mwakyembe.

Tunaamini utakuwa ‘Manny Pacquiao’ wa Tanzania, tuwe na Mwakinyo ‘Fist of the Nation’.

 

Drake, Meek Mill wawashangaza mashabiki
Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine