Na: Josefly Muhozi
Kwenye masimulizi mengi ya zamani, tumewahi kusikia wazee wakifunga na kuomba, walimuomba ‘Mungu wao’ awape mvua ili wasife kwa njaa, na mara nyingi kilio chao kilisikika wakapata mvua. Lakini wakati mwingine, mvua ilishuka kama gharika na kuwa chanzo cha vifo vingi. Yaani kama juu kuna koki ya maji, basi unaweza kusema kuna mtu alichomoa koki.
Wiki hii imekuwa changamoto kubwa kwa jiji la Dar es Salaam baada ya mvua kubwa kushuka na kusababisha mafuriko kwenye maeneo mengi. Madaraja mengi yameharibika na kusababisha maeneo mengi kutofikika. Nyumba kadhaa zimezama, mali zimeharibika na hata kusombwa na maji na wengine wamepoteza maisha.
Mwaka huu, kipindi cha On The Bench cha Dar24 Media kilipiga kambi kwenye eneo la Jangwani ambalo ni moja kati ya maeneo yanayokumbwa na mafuriko karibu kila mwaka, lakini wakaazi wake wengi wamegoma kuondoka ingawa Serikali iliwalipa fidia na kuwapa maeneo ya kuhamia.
On The Bench ya Dar24 iliwakutanisha wananchi na Maafisa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Afisa Mipango Miji. Mjadala ulileta elimu nzuri, lakini wapo walioshikilia msimamo kuwa hawatahama eneo hilo kwakuwa wanaamini ‘wanaletewa mafuriko’ ili wakimbie eneo hilo na watu wengine wakae. Hayo ndiyo mambo ya binadamu bwana. Imani na hisia huzaa mengi.
Lakini TMA iliwaeleza kuwa tahadhari inayotolewa wakati wa kiangazi ikipuuzwa majuto huja wakati wa mvua kwani hasara ya kupoteza maisha haiwezi kufidiwa. Hii ilinikumbusha simulizi la Nuhu aliyekuwa na umri wa miaka 500, ambaye aliwahimiza wananchi walioishi kwenye kiangazi muda mrefu kuingia kwenye Safina kwani ‘gharika’ linakuja, lakini wao wakapuuza. Majuto yalikuwa wakati mvua imeanza kunyesha na mlango wa Safina umefungwa. Kama hauifahamu kasome Biblia Takatifu, Mwanzo 6:9 na kuendelea. Au kasome Quran Takatifu Surah Al-Mu’minun [23:26]. Tena Quran Takatifu inasema kuna kijana mmoja wa Nuhu naye aliyakataa maelekezo ya baba yake ya kuingia kwenye Safina aliyoitengeneza akaamua kupanda mlimali, naye akazama.
Leo tujikumbushe tu majanga makubwa zaidi ya mafuriko katika historia duniani, ukiacha simulizi la gharika la Nuhu kwenye vitabu vitakatifu kabla ya kuzaliwa Kristo. China ilionekana kuongoza kwa matukio ya mafuriko makubwa zaidi duniani. Je, ni kwanini? Fuatilia hapa.
- Mafuriko ya Mto Yangtze – China, mwaka 1931
Hili linatajwa kuwa janga baya zaidi la mafuriko katika historia ya binadamu, lililotokea Agosti 18, 1931, lililosababisha vifo vya watu milioni 3.7, kufuatia mvua iliyonyesha kwa wingi na kwa kipindi kirefu. Maji yaliwalazimu watu zaidi ya laki tano kukimbia makazi yao.
Hata hivyo, chanzo kikuu cha vifo katika tuki hili haikuwa maji bali matokeo ya mafuriko. Vifo vingi vilitokana na njaa na magonjwa. Mashamba ya mchele yalisombwa na mafuriko na kusababisha njaa kali kwenye miji mikubwa ya Kusini mwa China. Pia, magonjwa mengi yaliibuka ikiwemo kipindipindu na typhoid; na kusababisha vifo vya watu wengi. Serikali ya China haikuwa imejipanga kukabiliana na hali hiyo kwakuwa ilikuwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe, hivyo madhara yalikuwa makubwa sana.
- Mafuriko ya Mto wa Njano (Yellow River), mwaka 1887
Mto Hwang Ho ulioko China, unaofahamika pia kwa lugha ya Kiingereza kama Yellow River, au kwa Kiswahili Mto wa Njano, unatajwa kuwa mto hatari zaidi kwa maisha ya binadamu. Kwa hali hiyo, unafahamika kwa jina la Kichina linaloweza kutafsiriwa kama ‘Huzuni ya China’. Hii ni kutokana na jinsi ulivyokuwa chanzo cha vifo vingi na uharibifu wa nchi.
Septemba 1887, mvua kubwa iliyomwagika ilisababisha Mto huo kufurika na watu milioni mbili waliyakimbia makazi yao. Mafuriko yalibeba eneo lenye ukubwa wa maili 50,000 za ardhi. Watu 900,000 walipoteza maisha ndani ya saa chache. Njaa na magonjwa nayo yalifuatana na kusababisha vifo vya maelfu ya watu; na inatajwa kuwa moja kati ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu.
- Mafuriko ya Mto wa Njano (Yellow River), mwaka 1938
Mafuriko yaliyoukabili tena Mto wa Njano (Yellow River), mwaka 1938 yalisababisha watu wengi waamini kuwa ingawa mafuriko yanafahamika kuwa ni janga la asili, haya yalichukuliwa kama sehemu ya vita.
Mafuriko haya yalikuja wakati ambapo China ilikuwa vitani ikipandana dhidi ya uvamizi wa Japan. Vita hiyo ilikuwa mbaya na ilitishia kuiondoa China kwenye ramani ya dunia na kuwa sehemu ya Japan.
Kutokana na kipigo walichokuwa wanapokea wachina dhidi ya Wajapan, kiongozi wa vita hiyo, Kamanda Chiang Kai-shek alifanya uamuzi mgumu. Aliamuru mfumo wa mto huo uvunjwe ili kuzuia Jeshi la Japan kuvuka kirahisi upande wa China. Hatua hiyo ilisababisha watu milioni nne kuyahama makazi yao baada ya mafuriko kusambaa. Maji yaliyotokana na mafuriko hayo yalisambaa kwa kipindi cha miaka tisa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira. Jeshi la China liliamua kuwatoa baadhi ya watu mhanga ili kuiokoa China yao dhidi ya wavamizi, inadaiwa kuwa waliamini hiyo ilikuwa moja ya nyenzo za vita!
Hata hivyo, China ilikuwa imekana kuwa ndiyo iliyotoa amri ya kuvunjwa kwa mfumo wa mto huo, hadi mwaka 1947, baada ya kuwashinda Wajapan. Serikali ya China ilikubali kuhusika baada ya habari kuanza kusambaa mwaka 1945 hadi 1947.
- Bwawa la Banqiao – China, 1975
Mwaka 1975, China ilipata pigo lingine, ni kama ilikuwa inaandamwa na mafuriko makubwa zaidi kuliko nchi nyingine. Mvua kubwa iliyoanza Agosti 5, 1975 ilishambulia ardhi ya Jimbo la Henan. Mvua hiyo nzito iliyoambatana na upepo wa kimbunga ilisababisha ndege wengi kupoteza maisha. Walipigwa na mvua yenye barafu na mizoga yao ilisambaa juu ya maji. Mtaani kwetu tunaita ‘mvua ya mawe’.
Mvua iliyonyesa siku moja tu ilizidi makadirio ya mvua iliyopaswa kunyesha kwa kipindi cha nusu mwaka. Kama juu kuna koki, basi kuna mtu alichomoa koki. Ikawa balaa. Siku ya pili mvua ilinyesha kwa saa 16 na siku ya tatu saa 13 bila kukoma.
Baada ya siku tatu, maji yaliyokuwa yanatunzwa kwenye Bwawa Banqiao yalifurika. Bwawa hilo lililokuwa limejengwa kuzunguka ‘Mto Ru’ lilizidiwa. Kutokana na wingi wa mvua iliyokuwa inaendelea kunyesha na kujaza ardhi, wafanyakazi wa bwawa hilo walipewa amri ya kutofungulia maji mengi kutoka kwenye huo mto. Kwa bahati mbaya, mvua hizo zilisababisha mawasiliano kukatika. Hivyo, wafanyakazi waliambiwa wanapaswa kuhisi tu nini cha kufanya kwani hakuna maelekezo watakayopata.
Usiku wa Agosti 8, 1975 ulikuwa usiku mbaya zaidi kwenye historia ya eneo hilo. Watu walikuwa wamelala huku mvua ya kawaida ikiendelea kunyesha. “Ghafla, ilisikika sauti mfano wa anga linapasuka,” alisema mtu mmoja aliyenusurika.
Ukuta wa Bwawa hilo lenye urefu wa mita 50 kwenda juu na upana wa maili kadhaa ulipasuka! Maji yaliyotoka kwenye Bwawa hilo yalisababisha mabwawa mengine 62 kupasuka pia. Usiku huo zaidi ya watu 26,000 walizama ndani ya maji na kupoteza maisha. Kwa ujumla, tukio hilo lilisababisha vifo vya watu takribani 230,000.
Lakini kitu kilichozua mjadala mkubwa kwenye tukio hilo la mafuriko ni kwamba inadaiwa lingeweza kuzuiwa. Inaelezwa kuwa mfanyakazi mmoja aitwaye Chen Xing alikuwa amewatahadharisha wakubwa zake kuhusu udhaifu unaoonekana kwenye kuta za bwawa hilo, lakini inaelezwa kuwa taarifa hiyo ilipuuziwa. Inaelezwa kuwa alitoa hadi mapendekezo ya namna ya kupata suluhu na kuondokana na hatari hiyo, lakini inadaiwa kuwa alituhumiwa kwa utovu wa nidhamu na kuondolewa kwenye mradi wa Bwawa hilo. Tahadhari yake ilikuwa kweli, ingefanyiwa kazi maisha ya maelfu ya watu yangeokolewa.
Miaka 11 baadaye, baada ya kufanya tafiti na kujiridhisha zaidi, Serikali ya China ilianza kujenga upya Bwawa hilo na lilikamilika mwaka 1993.
- Mafuriko katika Mto Yangtze, 1935
Mto Yangtze unatajwa kuwa chanzo cha mafuriko yote yaliyoikumba nchi ya China kwa asilimia 70 hadi 75, hasa kwa watu ambao wanaishi kando ya eneo la mto huo. Baada ya kushambuliwa na mafuriko ya mwaka 1931, mwaka 1935 ilikumbwa na pigo lingine la mafuriko ambapo takribani watu 145,000 walipoteza maisha na mamilioni walilazimika kuyahama makazi yao. Njaa na magonjwa yaliyoambatana na mafuriko hayo yalikuwa chanzo cha vifo vingi.
- Mafuriko ya St. Felix, 1530
Mafuriko yaliyoukumba mji wa St. Felix yanatajwa kuwa janga la mafuriko – baya zaidi kuwahi kutokea katika Bara la Ulaya. Mafuriko hayo yaliharibu kabisa na kufuta jiji la Kireno la Reimers Waal, ambao ulikuwa sehemu ya Dola ya Kirumi enzi hizo. Zaidi, vijiji vingine 18 vilifyekwa na maji kwa mvua iliyonyesha kwa siku moja. Jumamosi iliyoanza na utulivu ikaisha na maumivu. Baada ya tukio hilo, leo eneo hilo ni nyumba ya konokono na viwanda vingi vya uvuvi vimeanzishwa kuzunguka eneo hilo.
- Hanoi and Red River Delta Flood, 1971
Kufuatia shughuli nyingi za kijeshi na uharibifu wa mazingira, mafuriko yam Mto Delta, Kaskazini mwa Vietnam, yanatajwa kuwa moja kati ya majanga ya asili hatari zaidi katika historia ya Vietnam. Kwa bahati mbaya kutoka na mgogoro uliokuwa inaendelea kati ya Marekani na Vietnam, Serikali ya Vietnam ilizuia upatikanaji na utoaji wa taarifa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, janga hilo linakadiriwa kuwa lilisababisha vifo vya takribani watu 100,000.
Mafuriko hayo yalitokana na mvua kubwa iliyonyesha katika mji wa Hanoi kuanzia Agosti Mosi, 1971. Kwakuwa kulikuwa na pigo la vita, mvua na maradhi yatokanayo na mafuriko viliiumiza zaidi Vietnam.
- Mafurikio ya St. Lucia- Uholanzi, 1287
Mwaka 1287, kimbunga kikubwa kiliikumba Uholanzi na kusababisha mafuriko ambayo yalivyeka vijiji vingi na kusababisha vifo vya watu takribani 50,000.
Mafuriko hayo yalikuwa makubwa kiasi kwamba hata Kijiji cha Amsterdam (wakati huo) kilichokuwa kwenye nchi kavu, ghafla kiligeuka kuwa mji ulioko Pwani. Na hadi sasa jiji la Amsterdam liko ufukweni. Mafuriko hayo pia yaliathiri maeneo kadhaa ya Uingereza ingawa hakikuwa na madhara makubwa kulinganisha na upande wa Uholanzi.
- Mafuriko ya Mashariki mwa Guatemala, 1949
Hali ya hewa iliyobadilika ghafla na kukaribisha kimbunga kikali kutoka Kusini mwa Pwani ya Guatemala, kilisababisha moja kati ya majanga makubwa zaidi ya asili kuwahi kutokea katika eneo hilo, Septemba 27, 1949. Ingawa taarifa rasmi kuhusu janga hilo zimekuwa adimu, madhara ya mafuriko hayo yalikuwa yanaogofya. Inakadiriwa kuwa watu takribani 40,000 walipoteza maisha. Mafuriko hayo yalikuwa makubwa zaidi kwakuwa yalitokea wakati wa msimu wa kimbunga ulioanza kuipiga Marekani Kaskazini ukitokea Pwani za Atantic na Pacific.
- Mafuriko ya Bangladesh, 1974
Mvua kali iliyoshuka mfululizo na kusababisha mafuriko katika Mto Brahmaputra wa Bangladesh kati ya Aprili na Juni, 1974. Inakadiriwa kuwa takribani watu 28,700 walipoteza maisha katika siku za mwanzo tu za mafuriko hayo.
Kibaya zaidi, mafuriko hayo yalisomba mazao yaliyokuwa yanakaribia kuvunwa katika maeneo mengi nchini humo. Wakati huo Marekani ilikuwa imeiwekea vikwazo nchi hiyo hali iliyosababisha ishindwe kuagiza vyakula kutoka nchi kadhaa. Kutokana na hali hiyo, mamilioni ya wananchi walikumbwa na baa la njaa. Njaa hiyo iliyotokana na mafuriko inakadiriwa kusababisha vifo vya watu takribani milioni 1.5.
Watanzania, tuchukue hatua na kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Serikali, hasa kupitia TMA kwakuwa hivi sasa teknolojia inasaidia kuona kiwango cha mvua kinachoweza kunyesha katika siku za usoni. Pamoja na mambo mengine, tatizo kubwa ni ubishi wa watu wanapopewa tahadhari kwani wengi hupuuzia na kupeana moyo, umasikini, ubovu wa miundombinu, uduni wa makazi na rushwa.
Kwa Afrika Mashariki, kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita, mafuriko yaliyotokana na mvua iliyopewa jina la El Nino inatajwa kuwa ndiyo mvua iliyoleta madhara makubwa zaidi. El Nino imewahi kukumba ukanda huu mwaka 1982 na 1997/198 na kidogo mwaka 2015.
*Taarifa hizi zimetolewa katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mambo ya Binadamu (UN-OCHA), tovuti ya Timeline, tovuti ya ranker na tovuti ya thestreet.