Mazungumzo ya amani kati ya Serikali ya Ethiopia na wawakilishi wa Tigray imeendelea hii leo Novemba 10, 2022, huku Makamanda wa Kijeshi wakitoa maelezo kuhusu kupokonywa silaha kwa vikosi vya Tigray baada ya miaka miwili ya mzozo.
Afisa anayefuatilia mazungumzo hayo, amethibitisha suala hilo kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na kutoruhusiwa kuzungumza hadharani tangu kuanza kwake Jumatatu Novemba 7, 2022 nchini Kenya yalikuwa yamepangwa kukamilika jana siku Jumatano Novemba 9, 2022.
Mazungumzo hayo yanayoongozwa na Umoja wa Afrika AU, yanafuatia utiwaji saini wiki iliyopita wa usitishwaji mara moja mapigano katika mzozo ambao unakadiriwa kusababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu.
Umoja wa Mataifa UN, umesema bado wanasubiri kufika katika eneo hilo ili kutoa misaada ya chakula na vifaa muhimu vya matibabu kwa raia ambao wapo katika hali ya uhitaji.