Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais –Muungano na Mazingira, January Makamba amefafanua kuhusu namna alivyohojiwa na jeshi la polisi kuhusu sakata la kutekwa kwa Mohammed Dewji.
Kupitia akaunti yake ya Twitter, Makamba amekanusha taarifa zilizodai kuwa alikamatwa kwa ajili ya mahojiano, na badala yake amesema aliitwa kwa lengo la kutoa taarifa iliyohitajika kusaidia uchunguzi kwakuwa ni rafiki wa bilionea huyo.
“Ufafanuzi: Polisi walinipigia simu kuniomba, kama rafiki wa @moodewji, niwasaidie kama kuna chochote cha ziada ambacho Mo aliniambia kinachoweza kusaidia uchunguzi. Niliwaeleza. Wakasema kinafanana na alichowaeleza. Wakanishukuru. Wamefanya hivi pia kwa wanafamilia. Sikukamatwa,” Makamba ameandika.
Mapema leo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema kuwa Makamba alifika katika kituo cha polisi jana kwa ajili ya kutoa taarifa zilizohitajika kuhusu sakata hilo la utekaji.
“Alifika jana kwaajili ya kuchukuliwa maelezo kuhusiana na suala la kutekwa kwa mfanyabishara Mo Dewji, kuna mambo tulitaka kuyapata kutoka kwake kwaajili ya taarifa,” Mombasasa anakaririwa.
Mo alitekwa Oktoba 11 mwaka huu na alipatikana siku tisa baadaye baada ya watesi wake kumtupa katika eneo la Gymkhana jijini Dar es Salaam.
Jeshi la polisi limesema kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwabaini waliomteka bilionea huyo na kuwatia nguvuni.