Naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amewataka wananchi kutomsapoti mtu anaegawa fedha kwa nia ya kuingia ikulu kwa kuwa mtu huyo hafai kuiongoza nchi.

Makamba ameyasema hayo jana mjini Mtwara alipokuwa akikusanya sahihi za wadhamini kama sehemu ya kukidhi vigezo vya Chama Cha Mapinduzi katika kufanikisha kuwa mmoja kati ya majina ya watangaza nia watakaojadiliwa katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

“Mtu anayemwaga fedha na kuonesha mbwembwe nyingi hafai kuiongoza nchi kwa kuwa akiingia ikulu hatalisaidia taifa,” January Makamba anakaririwa.

Aidha, Makamba aliwaahidi wananchi wa Mtwara kuwa endapo atapata nafasi ya kuingia ikulu atahakikisha wananchi wanafaidika na zao la korosho. Pia, atahakikisha kuna miundo mbinu thabiti itakayosaidia kusafirisha mizigo katika sehemu mbalimbali za nchi kwa lengo la kukuza biashara na kuongeza kipato cha wananchi.

Katika hatua nyingine, Makamba alisema kuwa amejipanga kupokea matokeo yoyote na kwamba ataukubali uamuzi utakaofikiwa na CCM. Aliwashauri wagombea wenzake kuwa tayari kupokea matokeo yoyote na kueleza kuwa atakuwa tayari kukisapoti chama chake na mgombea atakayepitishwa.

Kesho (July 2, 2015) itakuwa mwisho wa kurudisha fomu kwa watangaza na baada ya muda zitafahamika mbivu na mbichi kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu.

Bendera Aipongeza Tff
Usain Bolt Awapa Ahuweni Wapinzani Wake