Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ameonya kuhusu matumizi ya nguvu wakati wa zoezi la udhibiti wa matumizi ya mifuko ya plastiki, baada ya tarehe ya ukomo wa matumizi yake.
Akizungumza katika kongamano la mijadala ya uwezeshaji wa matumizi ya mifuko mbadala uliohudhuriwa na makatibu tawala pamoja na watendaji wa serikali za mitaa, Makamba alisema kuwa utekelezaji wa sheria hiyo mpya unapaswa kufanywa bila kuwaumiza wananchi au kuingilia faragha zao.
“Tutapita kwenye maduka na magenge kuona kama watu wanatumia mifuko ya plastiki, na kama sheria inatekelezwa. Lakini hatutegemei kuwasimamisha watu na kuwapekua mifuko yao na mali zao; au mabegi yao kuona kama wana mifuko ya plastiki,” alisema Makamba.
“Unapoona mtu anautumia ndipo unapompiga faini kwa kufanya kosa na sio kumwambia hebu fungua gari tuone au fungua nyumba yako tuone kama unayo ndani,” aliongeza.
Aidha, Waziri Makamba alisisitiza kuwa hategemei kuona nguvu kubwa inatumika, kuwapiga virungu au kuwabeba juu-juu watu waliokutwa wakitumia mifuko ya plastiki wakiwemo akina mama na wazee, badala yake utoaji wa elimu uchukue nafasi kubwa zaidi.
Kadhalika, alionya hatua za kuchukua mali za watu waliokutwa wakitumia mifuko ya plastiki kama mbadala au dhamana ya malipo ya faini endapo hawatakuwa nayo.
Serikali imetangaza Juni Mosi, 2019 kama siku ya ukomo wa matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.