Waziri wa Nishati, January Makamba ametaka kupuuzwa kwa taarifa zinazosambaa mtandaoni tangu Juni 9, 2022, kuwa Serikali imepandisha bei ya umeme.
Akijibu swali la Mbunge wa Nyasa Stella Manyanya Bungeni jijini Dodoma hii leo Juni 10, 2022, Waziri Makamba amesema taarifa hizo si za kweli na Serikali imesikitishwa kwa uvumi huo wa uongo.
“Serikali imesikitishwa na wanaoeneza maneno ya uvumi kwenye mitandao na tumeomba Mamlaka husika zichukue hatua kwa udanganyifu unaofanywa,” amesisitiza Makamba.
Amesema, mchakato wa kupandisha bei ya Umeme unahusisha maombi ya Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), na Wananchi lazima washirikishwe katika utoaji wa maoni.
“Ni mchakato mrefu ambao hauwezi kufanyika kwa siri, kwahiyo hizi taarifa kwamba Serikali imepandisha bei ya umeme sio za kweli na ninaomba zipuuzwe,” amesema Waziri Makamba.
Katika baadhi ya machapisho ya mitandao ya kijamii, hapo jana Juni 9, 2022 yalionesha kupanda kwa bei ya Umeme hali ambayo iliyozua taharuki na baadhi ya watu kupinga juu ya suala hilo, wakidai kiwango kinachotangazwa kupanda kwa unit moja ni cha zamani.