Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba amesema kuwa Serikali haina mpango wa kutoa vibali kwa ajili ya kuuza shehena ya vinywaji aina ya viroba vilivyopo stoo kwenye maghala mbalimbali ya Wafanyabiashara wa pombe hiyo.
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam mara baada kufanya ziara ya kushtukiza katika ghala la Kampuni ya Usambazaji wa Vinywaji aina ya Viroba ya Temani iliyopo Kimara Temboni jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa Serikali ilitoa muda mrefu kuanzia mei 2016 mpaka machi 2017 kwa wenye shehena hiyo ya viroba kuuza na kumaliza mzigo wote uliopo stoo hivyo basi baada ya Serikali kupiga marufuku pombe hiyo, hakuna kibali kitakachotolewa kwa ajili ya kuuza shehena ya mzigo wa viroba uliobaki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Elizabeth Massawe amesema kuwa wanaiomba Serikali iwasaidie ili waweze kupunguza mzigo mkubwa wa viroba ambao wanao katika ghala lao sababu wanapata hasara kubwa na wanatakiwa kulipia kodi ya magahala waliyokodi.
Hata hivyo, Katika ziara hiyo ya kutembelea ghala la vinywaji la Kampuni ya Tema Enterprise, Makamba amejinea shehena kubwa ya katoni 150,000 za viroba zilizofungashiwa katika vifuko vya plastiki.