Uongozi wa Klabu ya Kitayosce FC (Tabora united) umedhamiria kumsajili Mshambuliaji wa Ihefu FC Yacouba Sogne pamoja na Mshambuliaji wa zamani wa Young Africans Herietier Makambo ili kuboresha kikosi cha klabu hiyo ambayo itashiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao 2023/24.

Kitayosce FC itashiriki Ligi Kuu msimu ujao ikitokea Ligi ya Championship sambamba na Mabingwa wa ligi hiyo JKT Tanzania, na sasa imeanza kujipanga kufanya usajili wa wachezaji wenye uzoefu na Mshike Mshike wa michuano hiyo mikubwa nchini Tanzania.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Adam Simba amesema wanataka kuwasajili Yacouba Sogne pamoja na Herietier Makambo ambao anaamini kuwa watawasaidia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa mwaka 2023/24.

“Kuhusu wachezaji hao, tayari tumesaini mikataba nao ya awali na tunasubiri michezo ya Ligi Kuu imalizike na dirisha la usajili lifunguliwe tukamilishe usajili wao,”

“Ukiachana na wachezaji hao tutasajili wachezaji wengine wakubwa wa ndani na nje ya nchi lengo letu likiwa ni kuhakikisha tunakuwa washindani wa Ligi Kuu msimu ujao na sio washiriki,” amesema Simba

Katika hatua nyingine kiongozi huyo amewataka mashabiki wa Kitayosce na watu wa Tabora kwa ujumla kutokuwa na mashaka kuhusu timu yao kutokana na mipango waliyonayo kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tukiwa kwenye Ligi ya Championship, ambayo haina udhamini timu yetu ndio timu pekee iliyokuwa ina wachezaji 12 wa kigeni, lakini tuliwalipa vizuri hadi mwishoni mwa msimu, hatuwezi kushindwa kuwalipa wachezaji wa kigeni tukiwa Ligi Kuu ambayo inawadhamini kibao,” amesema Simba

Kitayosce ambayo pia inajulikana kama Tabora United imepanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kumaliza nafasi ya pili ikiwa na alama 60 nyuma ya JKT Tanzania iliyokuwa na alama 63, huku Pamba ikimaliza nafasi ya tatu ikiwa na alama 59.

Lothar Matthaus afichua siri nzito Bayern Munich
Wajiri watakiwa kujisajili, kuwasilisha michango WCF