Ndoto za Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22 zinaemdelea kumsumbua Mshambuliaji kutoka DR Congo na Young Africans Heritier Makambo, ambaye tangu aliporejea klabuni hapo amekua akisisitiza anaitimiza ndoto hiyo.
Makambo amerejea Young Africans msimu huu, baada ya kuvunja mkataba na klabu ya AC Horoya ya Guinea, huku akiikuta klabu hiyo ikiendelea kusota na mpango wa kusaka ubingwa wa Tanzania Bara, ambao kwa mara ya nne mfululizo umechukuliwa na Simba SC.
Mshambuliaji huyo amesema matarajio yake ni kuona msimu huu wanafanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya wapinzani wao Simba SC, kwa kuwa wao wana kikosi imara na kina uwezo wa kupata matokeo kwenye mchezo wowote.
“Jambo kubwa ambalo lipo kwangu ni kuona naipambania timu kuweza kupata matokeo maana tunataka ubingwa wa msimu huu. Nataka kuisaidia timu kupata matokeo ikiwemo suala la kufunga mabao ndiyo kipaumbele kikubwa lakini kuona tunashinda kila mchezo kutokana na ubora wa timu yetu.”
“Tumewafunga Simba kwenye ngao lakini tunahitaji kuifunga pia kwenye ligi ili tuweze kufikia tunapotaka kwa kuweza kushinda kila mechi,” amesema Makambo.
Young Africans wameanza vizuri msimu huu 2021/22 kwa kushinda michezo yao miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama sita, wakiwatangulia wapinzani wao Simba SC kwa alama mbili, kufuatia mabingwa hao watetezi kushinda mchezo mmoja na kuambulia sare mchezo mmoja.