Licha ya kuonekana akipinga maamuzi ya mwamuzi Nassoro Mwichui kutoka mkoani Pwani baada ya kumuonesha kadi nyekundu, Kiungo wa Namungu FC, Abdulaziz Makame, ameonyesha uungwana baada ya kutafakari na kuona ipo haja ya kumwomba msamaha beki wa kulia wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba Shomari Kapombe, kutokana mchezo usio wa kiungwana.

Makame amesema haikuwa dhamira yake kucheza rafu hiyo bali lengo lake lilikuwa kutekeleza majukumu yake uwanjani kama mchezaji.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba radhi Watanzania na wapenda soka wote, kipekee zaidi nimwombe radhi mchezaji wa Simba, Shomari Kapombe kwa mchezo ambao sio wakiungwana, haikuwa dhamira yangu kumchezea rafu ni katika kutimiza wajibu wangu uwanjani kama mchezaji.”

“Mpira ni mchezo wa amani na tunashauriwa kucheza ‘Fair’, timu yangu ya Namungo chini ya kocha wangu, Morocco [Hemed] naomba radhi kwa kuigharimu timu yangu kucheza pungufu. Naahidi kuzidisha umakini katika michezo inayofuata,” aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Kumekuwa na matumizi makubwa ya nguvu yanayochangia wachezaji kutoonyesha mchezo wa kiungwana uwanjani hususan zinapocheza dhidi ya bingwa huyo mtetezi, Simba.

Kwa kuthibitisha hilo, kati ya michezo mitano ambayo Simba imecheza hadi sasa, mechi nne wachezaji wa timu pinzani wameonyeshwa kadi nyekundu.

Katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC dhidi ya Simba iliyopigwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Anuary Jabir alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya beki Kennedy Juma hadi kushindwa kuendelea na mchezo huo uliomalizika kwa Simba kushinda bao 1-0.

Kadhalika, wakati Simba ikishinda bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Juma Ramadhani naye alionyeshwa kadi nyekundu kwa rafu mbaya dhidi ya winga Bernard Morrison huku Benedictor Jacob Mwamlangwa wa Coastal Union naye akikumbana na adhabu hiyo, kabla ya Makame kwa Kapombe siku ya jumatano (Novemba 03).

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo, Simba ilishinda bao 1-0, shukrani kwa mtokea benchi Meddie Kagere aliyeifungia timu yake dakika za majeruhi.

Kwa matokeo hayo, Simba imepanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi nne nyuma ya vinara Yanga wenye alama 15 huku Namungo ikisalia na pointi zake tano hadi wakati huu timu zote zikiwa zimeshuka dimbani mara tano.

Tanzania na Norway kuongeza ushirikiano.
Rais Samia: Maalim Seif alikuwa ni makutano ya watu