Kiungo mkabaji wa Young Africans Abdulaziz Makame ‘Bui’ amesema changamoto ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza inamfanya azidi kupambana ili kumshawishi mkufunzi wa Young Africans Luc Eymael.
Makame alianza vyema maisha yake Young Africans akijihakikishia namba wakati mabingwa hao wa kihistoria wakinolewa na Mwinyi Zahera na baadae Charles Mkwasa kama kocha wa muda.
Hata hivyo tangu alipotua Eymael mwezi Januari mwaka huu, nafasi yake imekuwa finyu.
Kiungo huyo mwenye sifa ya kupiga pasi ndefu zenye uhakika, amesema alikaa nje kwa muda kutokana na kusumbuliwa na maradhi jambo lililomnyima nafasi ya kuonekana mwanzo na kocha Eymael wakati alipoanza majukumu yake.
Makame amesema sasa yuko sawa, tayari kupambana kuhakikisha anamshawishi Eymael kuweza kumjumuisha kwenye kikosi chake.
“Suala la mimi kutopata nafasi nalichukulia kama changamoto ya kunifanya nipambane zaidi. Matatizo ya kiafya ya kuumwa ni moja ya sababu iliyochangia kushindwa kumshawishi kocha kunipanga kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa kwa kocha aliyepita Mwinyi Zahera, “
“Bado naamini uwezo wa kila kocha kwa kuwa kila mmoja anakuja na mfumo na mbinu zake, mimi kama mchezaji natakiwa kupambana kutimiza majukumu yangu mazoezini na nina uhakika kurejea kwenye kikosi cha kwanza chini ya Eymael,” alisema Makame
Kiwango alichokuwa nacho mwanzoni mwa msimu kilimfanya kocha Etienne Ndayiragije amjumuishwe kwenye kikosi cha timu ya Taifa kilichofanikiwa kukata tiketi ya kushiriki fainali za CHAN zitakazofanyika Cameroon mwakani.
Baada ya kuondoshwa kwa taabu na Zesco United kwenye michuano ya ligi ya mabingwa raundi ya kwanza, Mkufunzi wa Zesco George Lwandamina alimtaja Bui kuwa ni miongoni mwa wachezaji waliomvutia kwenye kikosi cha Young Aficans.
Lwandamina aliyewahi kuinoa Young Aficans, alimtaja Bui kuwa mchezaji mwenye nafasi ya kufanikiwa kama ataendelea kujituma kutokana na umri wake bado kuwa mdogo.