Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, limewataka Walinzi wa Makampuni Binafsi ya ulinzi kuzingatia kanuni na taaribu za ulinzi wanapokuwa lindoni, ikiwa ni mkakati wa kuwakumbusha Askari wa Kampuni hizo kufuata utaratibu na wajibu wanaopaswa kutimiza wanapokuwa lindoni.

Akitoa elimu kwa Askari na Wamiliki wa Kampuni Binafsi za Ulinzi Wilayani Kasulu, Polisi Kata ya Kimobwa Mkaguzi msaidizi wa Polisi, Kokugonza Ally amesema Askari akiwa lindoni anatakiwa kuvaa sare, kuwa nadhifu, kutokuwa katika hali ya ulevi, kutokuondoka lindoni bila kutolewa na mtu unayemkabidhi lindo, kufanya ukaguzi wa lindo mara kwa mara, matumizi ya nguvu za kadri, kutokulala lindoni, umiliki na udhibiti sahihi wa silaha.

Amesema, pia Wamiliki wa Kampuni binafsi za ulinzi Wilayani humo wanatakiwa kutokuajiri Askari wa ulinzi wenye umri mkubwa, kuajiri askari wenye mafunzo ya Jeshi la akiba na kuwaleta askari wao mara kwa mara kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji kutoka Jeshi la Polisi.

Aidha wamiliki hao pia wametakiwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabiri askari hao ikiwemo maslahi madogo, kucheleweshewa malipo ya mshahara, ukosefu wa vitendea kazi, ukosefu wa muda wa mapumziko, changamoto ambazo zinaweza kuathiri utendaji kazi na kuhatarisha usalama wa mali wanazolinda.

Kwa upande wao wamiliki wa Kampuni binafsi za ulinzi wameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kufuata na kuzingatia miongozo,taratibu na maelekezo yote yanayotolewa na Jeshi la Polisi kuhakisha malindo wanayolinda yanaendelea kuwa salama.

Vijana wahamasishwe kufanya kazi kwa staha, uadilifu - Majaliwa
Matinyi arithi kiti cha Msigwa MAELEZO