Serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) imeyataja Makampuni matatu yatakayotumika kusafirisha Mashabiki wa Soka na Watanzania kwa ajili ya kuishangilia Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wakati wa Michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Mwezi Juni, mwaka huu nchini Misri.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo ambapo aliyataja Makampuni hayo kuwa ni pamoja na Clouds Entertainment Group Ltd, Travel Link na World Link, ambayo yalishinda mchakato wa ushindani na makampuni mengine kutokana na kukidhi vigezo mbalimbali vilivyoanishwa.
Kwa mujibu wa Singo amesema kuwa Serikali na kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) waliamua kusimamia mchakato wa kupata makampuni hayo ili kuzuia aina yoyote ya utapeli kwa Watanzania hususani Mashabiki wa Soka wa hapa nchini watakaojitokeza kwenda Nchini Misri kuipa nguvu ya ushingiliaji Taifa Stars.
“Katika miaka ya nyuma kulikuwa na utapeli katika haya makampuni ya usafirishaji, hivyo Serikali kwa kushirikiana na TFF tumeyapata Makampuni matatu, bei zao zitakuwa rahisi na wamepanga kuwa na nembo ya pamoja ambayo wataitangaza ili iweze kujulikana na Watanzania,” amesema Singo.
Aidha Singo amesema kuwa kuhusu utaratibu wa Visa za kusafiri makampuni hayo kwa kushirikana na TFF yatatoa taarifa ya jinsi Mashabiki wa Soka watakavyoweza kupata huduma hiyo kabla ya kuanza kwa michuano hiyo inayotarajia kuanza kutimua vumbi tarehe 21 Juni mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Clouds Entertainment Group Ltd, Shaffih Dauda amesema kuwa Kampuni yao imejipanga vyema kuhakikisha kuwa inatoa huduma zote muhimu kwa Watanzania watakaosafiri kwenda Nchini Misiri kuishangalia Taifa Stars ikiwemo visa, usafiri wa ndani, malazi katika kipindi cha siku 10 za mechi tatu za makundi itakayocheza Taifa Stars.
Kwa upande wake, Meneja Maendeleo ya Masoko wa Kampuni ya World Link, Zaki Admani amesema kuwa kampuni hiyo itatoza kiasi cha Dola za Kimarekani 1550 kwa Mashabiki wa Soka, ambao watasafiri kuelekea Nchini Misri pamoja na kutoa ofa ya kuchagua mechi moja yoyote ambayo mshabiki wa Soka atapenda kuiangalia katika timu zitakazochuana na Taifa Stars.
-
Waziri Makamba kuongoza Operesheni ya kukusanya Mifuko ya Plastiki
-
Wananchi wajitolea kujenga Barabara
-
Video: Sirro amhakikishia usalama Tundu Lissu, RC aamuru watumishi kusalimisha kadi za ATM, Lugola asimamisha wakuu wa polisi wilayani Geita
Naye Meneja Utawala wa Kampuni ya Travel Link, Ephraim Mtuya amesema kuwa kwa miaka 15 sasa Kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi pamoja na TFF kwa ajili ya kuwasafirisha wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania katika nchi mbalimbali na hivyo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kusafiri na Kampuni hiyo ili kwenda kuipa nguvu Timu ya Taifa ya Tanzania ikiwa nchini Misri.