Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Faustine Ndugulile ameipa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) miezi mitatu kumaliza changamoto za bando na vifurushi zinazotolewa na kampuni za simu za mkononi kwa wananchi.

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TCRA ikiwa ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kufahamiana, kushirikiana kwa kufanya kazi kwa pamoja katika kuhudumia wananchi kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa kidijitali.

Ameongeza kuwa TCRA ishughulikie malalamiko ya wananchi kwa kuwa wananchi hawana imani na vifurushi na bando, na kuwe na mfumo wa kuhakiki gharama halisi za mawasiliano kuendana na fedha aliyotoa mwananchi.

Aidha, amehimiza wahakikishe kuwa chaneli tano za bure za runinga zinaonekana hata baada ya muda wa kulipia kumalizika kwa kuwa chaneli hizo hazionekani kwenye baadhi ya ving’amuzi.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew ameipongeza TCRA kwa kutengeneza mifumo ya TEHAMA, kutambua changamoto zilizopo na imejipanga kuzifanyia kazi kwa kuwa lazima TEHAMA ichukue nafasi yake na itufikishe watanzania tunakotaka kwenda.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amewataka wafanyakazi wa TCRA kujiongeza na kujituma zaidi badala ya kusubiri maagizo na maelekezo kwa kuwa wao ni wataalamu.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amekiri uwepo wa changamoto za bando na vifurushi na ameahidi kuzifanyia kazi kwa kuwa TEHAMA imeongeza mnyororo wa thamani kwenye sekta zote na imesogeza huduma mbali mbali viganjani.

Jembe Ulaya amshauri Sven Vandenbroeck
Ruto akataa kumuunga mkono Mudavadi urais